Wakana Mungu wamkaribisha mwimbaji ambaye pia ni mhubiri Ruth Matete

Jamii ya wakana Mungu nchini Kenya au ukipenda “Atheist Society of Kenya” imemkaribisha Ruth Matete ambaye huimba nyimbo za injili na ambaye pia amehitimu kama muhubiri.

Kiongozi wa jamii hiyo ya wakana Mungu kwa jina Harrison Mumia alimhimiza Ruth aachane na dini kabisa ndipo apate kutulia.

“Ningependa kumwambia Ruth kwamba nilikuwa mkristo kama yeye na nikaona unafiki kanisani. Wakristo hujionyesha kama watu wenye upendo, haki na amani vitu ambavyo kwa kweli haviko katika maisha yao.” aliandika Mumia.

Mumia anasema imekuwa miaka 20 tangu aachane na dini na amekuwa akiishi kwa amani.

Hii ni baada ya Ruth kuonyesha kutoridhika kwake na watu ambao ni waumini kama yeye ambao aliwachukulia kuwa marafiki kumtoroka alipopata shida na wakamhukumu.

Ruth alifiwa na mume wake BelovedJohn Apewajoye ambaye pia alikuwa mhubiri baada ya ajali ya nyumbani iliyotokana na mlipuko wa gesi ya kupikia.

 

Baada ya hapo kukatokea video ya mtu fulani wa asili ya Nigeria, alikozaliwa BelovedJohn, akidai kwamba Ruth anafaa kuambia ulimwengu ukweli kuhusu kifo cha mume wake.

Jambo hilo lilisababisha mvutano kati ya Ruth na jamii ya watu wa asili ya Nigeria nchini hadi kukatolewa maagizo ya mahakama ya kuzuia kuzikwa kwa mwili wa mumewe Ruth.

Hatimaye mzozo ulitatuliwa akakubaliwa kuuzika.

Ruth amerejea kwenye mitandao ya kijamii maajuzi tu na tarehe 19 mwezi Septemba mwaka 2020 aliandika makala marefu akionyesha kutoridhika na jinsi watu wa karibu walimhukumu, wakamtenga na sasa wamerudi kwake tena baada ya kile ambacho anasema ni Mungu kuthibitisha ukweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *