Wajane wa Murunga waitaka mahakama iwaruhusu wamzike mume wao

Wajane wawili wa marehemu mbunge wa Matungu Justus Murunga wameiomba mahakama iwaruhusu wamzike marehemu mume wao huku wakisubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na mwanamke mmoja anayedai kuwa mkewe.

Christabel na Grace Murunga sasa wanaitaka mahakama itupilie mbali rufaa hiyo ya Agnes Wangui ambayo ilisababisha kusitishwa kwa mazishi hayo kwa muda.

Wangui alisitisha mipango ya mazishi kusubiri matokeo ya uchunguzi wa msimbo jeni au DNA kubaini iwapo watoto wake wawili ni wa marehemu mbunge huyo.

Wajane hao wawili kupitia kwa wakili wao Patrick Lutta walisema kuendelea kuahirishwa kwa mazishi ya mume wao kunazua taharuki isiyofaa kwani uzazi wa watoto hao unaweza kubainishwa kupitia uchunguzi wa DNA.

Wangui anadai kwamba yeye na marehemu mbunge huyo walikuwa na uhusiano na walikuwa na mipango ya kurasimisha ndoa yao.

Mazishi ya marehemu Murunga yalikuwa yafanyike tarehe 28 mwezi huu wa Novemba lakini yakasitishwa na agizo la mahakama baada ya mwanamke mmoja kudai kuwa ana watoto wawili na marehemu mbunge huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *