Wahudumu wa Bodaboda waonywa dhidi ya kujihusisha na uhalifu

Mwenyekiti wa chama cha wahudumu wa bodaboda mjini Machakos, Allan Musembi ametoa onyo kali kwa wahudumu wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Musembi amesema kuwa wale wanaojificha kwenye biashara hiyo huku wakitekeleza uhalifu watasakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Ameonya kwamba wahudumu watakaopatikana wakiwapora wateja hawatavumiliwa.

Musembi amefichua kuwa baadhi ya wahudumu wa bodaboda wasio waaminifu wamehusishwa na vitendo vya uhalifu.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa wanaofanya hivyo wanaharibu sifa ya kazi hiyo ambayo ni kiini cha riziki kwa vijana wengi.

“Nataka niwahimize wazazi wawatahadharishe vijana wao ambao ni wahudumu wa bodaboda wakome kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwa sababu chama chetu hakitaruhusu wahudumu wachache kuharibu sifa yetu,” akasema.

Musembi alikuwa akiongea baada ya chama hicho kumkamata na kumkabidhi kwa polisi mhudumu mmoja aliyekuwa ameiba simu na dawa kutoka kwa abiria wake.

“Tulipopokea ripoti hiyo tulihamasisha wahudumu wengine waliomsaka na kumkamata katika eneo la Kameo huko Mumbuni.”

Mshukiwa huyo anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Machakos akisubiri kufikishwa Mahakamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *