Wahariri wadai Uhuru wa vyombo vya habari unavurugwa

Chama cha wahariri humu nchini kimesema kitawasilisha ombi kwa bunge la kitaifa kushinikiza utekelezaji wa uhuru wa vyombo vya habari kwa manufaa ya Wakenya na haki za kidemokrasia.

Haya yamejiri huku mzozo ukiendelea kutokota kufuatia juhudi za kuondolewa kwa Tabitha Mutemi kutoka kwa baraza la vyombo vya habari.

Kwenye taarifa, chama hicho kinasema kuingilia uadilifu wa baraza hilo ni tisho kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Kulingana na chama hicho suala hilo liliibuliwa tarehe 11 mwezi Januari mwaka huu wakati afisa mkuu mtendaji wa chama hicho David Omwoyo, alipomwandikia mwenyekiti Maina Muiruri, kumfahamisha kuwa Mutemi hatambuliwi tena kama mwanachama wa bodi ya chama cha wahariri humu nchini.

Omwoyo alifahamisha baraza hilo kwamba alipokea ushauri kutoka kwa mwanasheria mkuu ulioashiria kuwa uteuzi wa Mutemi ulikuwa kinyume cha sheria kwani tayari anashikilia wadhifa mwingine katika tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini.

Mwenyekiti wa chama cha wahariri humu nchini Churchill Otieno hata hivyo alisema kuondolewa kwa Mutemi ni kinyume cha sheria. Churchill alitoa wito wa mashauriano ili kudumisha hadhi ya baraza la vyombo vya habari nchini.

Mutemi alikuwa ameteuliwa baada ya kufanya vyema wakati wa mahojiano yaliyofanywa na jopo lililoteuliwa na wadau na kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali na waziri wa habari Joe Mucheru, kama mwanachama wa bodi ya chama hicho, tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2019.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *