Categories
Habari

Wafanyibiashara wa Soko la Mung’etho huko Kiambu walalamikia unyakuzi wa ardhi ya soko lao

Zaidi ya wafanyibiashara wadogo 500 katika soko la Mung’etho huko Juja, Kaunti ya Kiambu wamelalamika kuhusu njama ya wastawishaji wa kibinafsi kunyakua sehemu ya soko hilo la ekari tano ambayo wamekuwa wakitumia kuendesha bishara zao.

Kipande hicho cha ardhi kilicho karibu na Chuo Kikuu cha JKUAT kimekua kikizozaniwa na pande hizo mbili kwa muda wa miaka miwili sasa.

Wafanyibiashara hao tayari wamepokea ilani ya kutimuliwa, hatua ambayo imezua hofu miongoni mwao.

Wafanyibiashara hao walionyesha stakabadhi za kubaini kuwa tayari kipande hicho cha ardhi kimenyakuliwa na nyumba za kukodishwa kujengwa mahala hapo.

“Hii shamba yetu tunataka kunyang’anywa, tutaelekea wapi? Gavana wetu Nyoro usikie kilio chetu ili wale wanaotaka kuchukua hii ardhi wajue hili soko ni la serikali na ni letu,” amelalamika mmoja wa wafanyibiashara hao.

Kulingana na Edwin Nderitu, Mwenyekiti wa soko hilo, wanyakuzi hao tayari wameuza ardhi hiyo.

Wafanyibiashara hao wametoa wito kwa Gavana wa Kauti ya Kiambu James Nyoro kuingilia kati swala hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *