Waathiriwa waliopoteza makazi kufuatia kimbunga cha Eloise nchini Msumbiji wakusanyika Guara Guara

Mamia ya wakazi wa Wilaya ya Buzi nchini Msumbiji wamekita kambi katika kituo cha utawala cha Guara Guara wakisuburi kuopolewa baada ya makazi yao kuharibiwa na kimbunga kwa jina Eloise.

Baadhi ya wakazi hao wanasema wamekuwa mahali hapo kwa muda wa siku tatu sasa.

Shirika la kitaifa la kukabiliana na majanga linasema juhudi zinafanywa kuhakikisha kila mtu anaokolewa.

Wanaookolewa wanapelekwa katika nyumba za watu binafsi huku wengine wakipelekwa katika vituo wanakopata hifadhi.

Shughuli ya kuwahamisha wakazi ilianza tarehe 20 mwezi huu, siku tatu kabla ya kuwasili kwa kimbunga cha Eloise kilichoandamana na upepo uliovuma kwa kasi ya kati ya kilomita 120 na 150 kwa saa na mvua kubwa iliyozidi milimita 200 kwa muda wa saa 12.

Taasisi ya kitaifa ya majanga imesema wengi wa wakazi walikaidi onyo lililotolewa kuwataka kuhama ambako watu wa kwanza kuokolewa walipelekwa katika kituo cha utawala cha Guara Guara kwa lazima.

Haijabainika itachukua muda gani kuwahamisha wakazi wote kwani wanaendelea kumiminika katika kituo hicho cha utawala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *