Waasi washambulia kambi moja ya kijeshi nchini Cameroon

Maafisa wanne wa kijeshi wameuawa kwenye shambulizi la waasi dhidi ya kambi moja ya kijeshi magharibi mwa nchi ya Cameroon.

Jimbo hilo,ambalo wakazi wake wengi wanatumia lugha ya kiingereza,  limeshuhudia harakati za waasi wanaolitaka kujitenga.

Kiongozi wa waasi hao Mark Bareta, alipakua picha kwenye mtandao wa Facebook, akisema shambulizi hilo ni la kulipiza kisasi kutiwa nguvuni kwa raia watatu wa jimbo hilo na jeshi la nchi hiyo.

Kiongozi mmoja kutoka eneo la magharibi mwa wilaya ya Ngalim, alithibitisha kutekelezwa kwa shambulizi hilo dhidi ya kituo cha kijeshi cha Menfaoung, japo hakutoa maelezo zaidi.

Jimbo hilo, hasa maeneo ya Menoua na Bamboutos yamekuwa yakilengwa mara kwa mara na waasi hao.

Umoja wa mataifa unakadiria kwamba takriban watu 3,500 wameuawa katika maeneo ya kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa jimbo hilo tangu waasi walipoanzisha harakati za kutaka kujitenga mwaka wa 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *