Visa 949 vipya vya Covid-19 vyanakiliwa huku watu wanne zaidi wakifariki

Kenya imenakili visa 949 vipya vya ugonjwa wa  covid-19 kufuatia kupimwa kwa  sampuli 8,311 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Idadi hiyo inafikisha 82,605 jumla ya visa vya Covid-19 vilivyothibitishwa humu nchini hadi sasa.

Kwenye taarifa waziri wa afya Mutahi Kagwe, alisema kuwa jumla ya sampuli zilizopimwa kufikia sasa ni 879,261.

Kagwe alisema  kati ya visa hivyo vipya, 913 ni wakenya huku 36 wakiwa raia wa kigeni.

Alisema kuwa 558 ni wanaume na 391 ni wanawake. Wathiriwa wenye umri mdogo zaidi ni mtoto mchanga wa miezi miwili na mzee zaidi ana umri wa miaka 100.

Kaunti ya Nairobi imeendelea kuongoza kwa idadi ya visa huku ikinakili visa  400 ikifuatiwa na Kiambu kwa visa 138, Mombasa visa 71, Kakamega visa 49, Kericho visa 33 na Kisii visa 30.

Kaunti ya Nyamira iliandikisha visa 26, Machakos visa 24, Kisumu visa 18, Kilifi visa 15, Taita Taveta visa 15, Bungoma visa 15, Busia visa 14, Makueni, Siaya, Kajiado, Turkana, na Laikipia visa 9 kila moja. Embu visa 8, Murang’a visa 7 na Nyeri visa 7.

Wagonjwa 274 zaidi wamepona kutokana na ugonjwa huo ambapo 224 walikuwa kwenye mpango wa utunzaji wa nyumbani huku 50 wakiondoka kweney hospitali mbalimbali.

Jumla ya idadi ya wale waliopona kufikia sasa ni 54,399.

Hata hivyo wagonjwa  4 zaidi wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo na kufikisha 1,445 idadi jumla ya wale walioaga dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *