Visa 400 vipya vya Covid-19 vyanakiliwa hapa nchini

Visa 400 vipya vya Covid-19 vimenakiliwa hapa nchini baada ya kupimwa kwa sampuli 5,189 katika muda wa saa 24 zilizopita.

Kupitia kwa taarifa, waziri wa afya Mutahi Kagwe alisema idadi jumla ya visa vilivyothibitishwa hapa nchini sasa ni 107,729 kutoka kwa idadi jumla ya sampuli 1,322,806 zilizochunguzwa.

Kati ya visa hivyo 400, visa 367 ni vya raia wa kenya ilhali 33 ni vya raia wa kigeni ambapo  248 ni wa kiume na 154 ni wa kike.

Mwathiriwa mchanga zaidi ni mtoto wa umri wa miezi minane huku mkongwe zaidi akiwa na umri wa miaka 95.

Kaunti ya Nairobi ilinakili visa 279, Kiambu 37, Murang’a 9, Kericho 9, Kajiado 8, Machakos 7 huku Kisumu, Turkana na Nyeri zikiandikisha visa 6 kila moja.

Kaunti ya Busia na Uasin Gishu zilinakili visa 4 kila kaunti huku Garissa, Kilifi na Kitui zikiwa na visa 3 kila moja.

Kisii, Makueni, Siaya, Vihiga,Mombasa na Nakuru zilikuwa na visa 2 kila moja huku Nandi, Nyandarua, Bomet na Bungoma zikiwa na kisa kimoja kila kaunti.

Hata hivyo watu watatu zaidi wamefariki kutokana makali ya Covid-19 na kufikisha idadi jumla ya vifo kutokana na Covid-19 hapa nchini kuwa 1,873. 

Wakati huo huo wagonjwa wengine 77 wamepona virusi hivyo hatari ambapo 50 walitoka katika hospitali mbali mbali humu nchini na 27 walitoka katika ule mpango wa kuwahudumia wagonjwa nyumbani.

Idadi jumla ya waliopona covid-19 hapa nchini kulingana na wizara ya afya sasa ni  87176. 

Kagwe aliongeza kuwa wagonjwa 494 kwa sasa wamelazwa katika hospitali mbali mbali nchini huku wengine 1,615 wakihudumiwa nyumbani.

Wagonjwa 67 wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ambapo 24 wanatumia vipumulio na 35 wanapokea hewa ya ziada ya oxygen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *