Visa 138 vipya vya Covid-19 vyanakiliwa humu nchini

Visa 138 vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 vimenakiliwa hapa nchini na kufikisha idadi jumla ya maambukizi kuwa 98,693.

Visa hivi vipya vinatokana na sampuli 4,526 zilizopimwa katika muda wa saa 24 zilizopita. Kati ya visa hivyo 119 ni vya Wakenya na 19 ni vya raia wa kigeni.

Mwathiriwa mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto wa mwaka mmoja ilhali yule mwenye umri mkubwa zaidi ana miaka 80.

Nairobi inaendelea kuongoza kwa visa vya maambukizi ikiwa na visa 65 ikifuatiwa na Kericho kwa visa 23 na Mombasa visa 10.

Hata hivyo wagonjwa 266 zaidi wamepona ugonjwa huo, 251 chini ya ule mpango wa utunzi wa nyumbani na 15 wameruhusiwa kuondoka katika hospitali mbali mbali.

Idadi jumla ya wagonjwa waliopona sasa imefikia 81,933.

Wakati huo huo wagonjwa watatu zaidi wameaga dunia baada ya kuambukizwa ugonjwa huo na kufikisha idadi jumla ya waliofariki kuwa 1,723.

Kwa sasa kuna wagonjwa 680 ambao wamelazwa katika hospitali mbali mbali, ilhali wengine 1,730 wamejitenga chini ya mpango wa utunzi wa nyumbani.

Wagonjwa 26 wamelazwa katika vitengo vya wagonjwa mahututi ambapo 17 kati yao wanatumia vipumulio na 8 wanapokea oksijeni ya ziada.

Mmoja amewekwa chini ya uchunguzi. Wagonjwa watatu wako katika kitengo cha kutoa matibabu maalum.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *