Viongozi wanawake kaunti ya Kitui wataka nyadhifa zaidi kupitia BBI

Wabunge wanawake katika kaunti ya Kitui wamesema watachunguza kwa makini ripoti ya mpango wa maridhiano ya BBI ili kuhakikisha haihujumu juhudi zilizoafikiwa za kuwawezesha wanawake humu nchini.

Wakizungumza wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku kuu ya mashujaa katika eneo la Mutomo, wabunge hao Dkt Rachael Kaki Nyamai wa kitui kusini na Dkt Irene Kasalu ambaye ni mwakilishi wanawake, walisema nyadhifa za wanawake ambazo zimeratibiwa ndani ya katiba ya mwaka 2010 zinapaswa kudumishwa.

Waliongeza kuwa mpango wa BBI unapaswa kuongeza nafasi zaidi za wanawake ili kuhakikisha uakilishi wa kisiasa wa wanawake dhidi ya wanaume ni asilimia 50 kwa 50.

Mwakilishi wanawake kaunti ya Kitui Dkt. Irene Kasalu kwa upande wake alisema ili wanawake waunge mkono ripoti ya BBI, ni sharti ripoti hiyo ishughulikie maswala kama vile uwakilishi wa kijinsia wa thuluthi mbili sawia na kuboresha maslahi ya wanawake nchini.

Dkt. Kasalu alisema wanawake lazima wapewe kipaumbele katika ripoti hiyo ya BBi la sivyo hataiunga mkono.

Naye mbunge wa Kitui kusini Dkt. Rachael Kaki Nyamai alisema anaimani kuwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga watahakikisha BBI inashughulikia maswala ya wanawake  na kwamba nafasi zaidi za wanawake zinabuniwa.

Wakati uo huo Dkt. Nyamai alitoa wito kwa Rais uhuru Kenyatta kuhakikisha Amani inadumu humu nchini kabla na baada ya uchaguzi mkuu ujao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *