Viongozi wa vijana Nairobi waapa kuandamana wakipinga kubanduliwa mamlakani kwa Sonko

Baadhi ya vijana wa Kaunti ya Nairobi wameshtumu vikali hatua ya kubanduliwa mamlakani kwa Gavana Mike Mbuvi Sonko.

Sonko aliondolewa afisini na wanachama wa Bunge la Kaunti hiyo siku ya Alhamisi kwa madai ya utumuzi mbaya wa mamlaka, utovu wa nidhamu na kukosa uwezo wa kimwili na kiakili kuendesha maswala ya Kaunti hiyo.

Kupitia kwenye mwavuli wa mashirika ya mashinani ya kutetea haki za binadamu, viongozi wa vijana wameapa kukaidi hatua ya kumbandua Sonko uongozini wakisema ilitekelezwa bila kuzingatia sheria.

Vijana hao wametangaza mpango wa kufanya maandamani hadi katika makao makuu ya kaunti hiyo na pia Bunge la Seneti wiki ijayo ili kuonyesha gadhabu yao kutokana na hatua ya kubanduliwa kwa Sonko.

Gavana huyo wa Nairobi anayekabiliwa na matatizo anatarajiwa kufika mahakamani kesho kupinga utaratibu uliotumiwa kumwondoa afisini, akisema ulikuwa na kasoro chungu nzima.

Aidha, Sonko angependa kuwataja Katibu na Spika wa Bunge la Kaunti hiyo Ben Mutura, kwa kudharau maagizo ya mahakama, waliporuhusu kujadiliwa kwa hoja ya kumwondoa mamlakani ilhali  kulikuwa na maagizo ya kusitisha utaratibu huo.

Siku ya Alhamisi, wanachama 88 wa Bunge la Kaunti ya Nairobi walipiga kura na kupitisha mswaada wa kumuondoa Sonko mamlakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *