Viongozi wa KNUN Muranga, Kiambu na Nyeri matatani kwa kuwakataza wauguzi kushiriki mgomo

Chama cha Kitaifa cha Wauguzi kimesema kitawasimamisha kazi wawakilishi wa chama hicho katika kaunti za Muranga, Kiambu na Nyeri kwa kuwanyima wanachama wao haki ya kushiriki kwenye mgomo unaoendelea wa wauguzi.

Akiwahutubia waandishi wa habari jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako amesema kuwa wakuu wa chama hicho katika kaunti hizo tatu watapokonywa majukumu yao iwapo watakosa kuwaruhusu wanachama hao kujiunga na wenzao kwenye mgomo kufikia Jumatano jioni.

Panyako amesema ni makosa kwa wawakilishi hao kuwanyima wanachama wao haki ya kushinikiza kuimarishwa kwa maslahi yao pamoja na wenzao katika kaunti nyingine ambao wangali wamegoma.

Panyako ameelezea imani kwamba mashauriano yanayoendelea na serikali kuhusiana na shinikizo zao yatakomesha mgomo huo hivi karibuni.

“Wale viongozi ambao wamesababisha wafanyikazi wasianze mgomo katika hizo kufikia jioni ya leo watakuwa wamesimamishwa kama viongozi wa chama hiki na tutaweka kaimu viongozi katika kaunti hizo ili kuendesha shughuli za chama hiki,” amesema Panyako.

Wakati uo huo, wahudumu wa afya katika Kaunti ya Makueni waliokuwa wamegoma kudhihirisha umoja na wenzao wamesitisha mgomo katika kaunti hiyo kwa muda wa siku 30 zijazo.

Uamuzi huo uliafikiwa baada ya viongozi wa kaunti hiyo kusema watashughulikia shinikizo zao katika muda wa siku  30 zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *