Viongozi wa kaunti ya Nakuru: Hatutakubali umwagikaji wa damu tena

Viongozi katika kaunti ya Nakuru wameunga mkono tangazo la Rais Uhuru Kenyatta kwamba kesi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, hazitafufuliwa.

Wakiongea katika eneo la Naivasha baada ya kukutana na tume ya mshikamano wa kitaifa NCIC, viongozi hao wakiwemo wabunge Jane Kihara wa Naivasha, Kimani Ngunjiru wa Bahati pamoja na mwakilishi wa wanawake kaunti ya Nakuru Liza Chelule walidai kuwa baadhi ya wanasiasa wenye nia mbaya  ndiyo waliohusika na jaribio la kufufua kesi hizo wakisaidiwa na kitengo cha DCI.

Kulingana na mbunge wa Naivasha Jane Kihara, baadhi ya waliokuwa wakimbizi wa ndani kwa ndani walishawishiwa na mbunge mmoja maalum kuandikisha upya taarifa kuhusu ghasia hizo.

“Tunafahamu kuwa mbunge mmoja mteule ambaye amekuwa akiwashawishi wakimbizi wa ndani kwa ndani kuandikisha taarifa kwa malipo. Kinoti anapaswa afanye kazi yake na ajiepushe na siasa,” alifoka Kihara.

Kwa upande wake mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri aliwalaumu watu kutoka nje ya kaunt hiyo kwa kujaribu kusababisha vurugu katika kaunti ya Nakuru kupitia taarifa zisizo na msingi wowote.

“Tunawajua wanaoshinikiza hatua hii mpya lakini kama viongozi wa Nakuru tumeapa kuhakikisha hakuna umwagikaji wa damu kupitia siasa duni,”alisema Ngunjiri.

Akiongea, mwenyekiti wa tume hiyo ya utangamano na mshikamano wa kitaifa kasisi Samuel Kobia alisema wanashirikiana na viongozi  kuhakikisha amani inadumishwa.

“Tunaelekea katika kipindi cha siasa na tuko makini kushirikiana na viongozi pamoja na wazee kuhakikisha amani inadumishwa wakati wote,” alisema Kobia.

Siku ya jumatano rais Kenyatta alikosoa jaribio la kufufua kesi hizo akionywa kuwa huenda ikavuruga amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *