Vikosi vya Ethiopia vyashambulia jiji kuu ya Tigray,Mekelle

Vikosi vya serikali nchini Ethiopia vimetekeleza shambulizi kali katika jiji kuu la eneo la Tigray kaskazini ya nchi hiyo kwa mujibu wa wahudumu wa mashirika ya utoaji misaada na maafisa wa eneo hilo.

Chama tawala katika eneo hilo kimesema kuwa eneo la katikati ya jiji la Mekelle limeshambuliwa kwa silaha hatari na mizinga.

Jeshi la Ethiopia limekuwa likikabiliana na kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kwa majuma kadhaa.

Limesema linatumai kukomboa jiji hilio kutoka kwa kundi la TPLF katika muda wa siku chache zijazo lakini litaepusha kuwadhuru wakazi wake nusu milioni.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa na maelfu ya wengine kulazimika kutoroka makazi yao huku vikosi vya Ethiopia vikitwaa miji.  

Awali jeshi la Ethiopia lilisema kuwa limekomboa mji wa Wikro, ulio kaskazini ya Mekelle, pamoja na miji mingine katika eneo la Tigray.

Ni vigumu kuthibitisha habari kuhusu mapigano hayo kwani mawasiliano yote ya simu zikiwemo zile za rununu na mtandao katika eneo la Tigray yamekatizwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *