Vijana wa ODM huko Pwani waapa kupambana na waasi wa chama hicho

Viongozi wa vijana katika chama cha ODM Ukanda wa Pwani, wamepinga vikali wito wa kuundwa kwa chama cha kisiasa cha Pwani unaotolewa na viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Vijana hao wamesema eneo hilo ni ngome ya ODM na wakaapa kulilinda kutokana na wenye nia ya kulivamia na kugawanya wakazi kisiasa.

Wamesema haya kwenye mkutano na wajumbe wa ODM kutoka eneo zima la Pwani uliofanyika katika Ukumbi wa Arabuko Sokoke Jamii Villas, Kaunti ya Kilifi.

Wamewakashifu wabunge Owen Baya wa Kilifi Kaskazini na Aisha Jumwa wa Malindi kwa kampeni zao za kushinikiza kuundwa kwa chama kipya cha Pwani na pia wakaapa kutwaa ushindi kwenye chaguzi tatu ndogo zijazo katika eneo hilo.

Chaguzi hizo ni ule wa Ubunge wa Msambweni Kaunti ya Kwale na Uwakilishi Wodi za Dabaso na Wundanyi katika Kaunti za Kilifi na Taita Taveta mtawalia, ambazo zimeratibiwa kufanyika tarehe 15 Desemba mwaka huu.

Wamemsihi kinara wa ODM Raila Odinga na naibu wake Ali Hassan Joho watulie na kuwapa nafasi vijana hao wadhihirishe ubabe wao wa kisiasa katika chaguzi hizo tatu ndogo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyosomwa naye Mwenyekiti wa Vijana wa ODM Kaunti ya Taita Taveta Patricia Mwashighadi, vijana hao wameamua kuwa katika msitari wa mbele kwenye chaguzi hizo.

“Chama cha ODM kimekita mizizi katika eneo la Pwani, kinaazimia kuleta mafanikio kwa wananchi na kimestahimili changamoto za kutetea haki zao,” amesema Mwashighadi katika taarifa hiyo.

Mwashighadi ameongeza kuwa vijana hao wameazimia kuzuru nyanjani kwa zoezi la kusajili wakazi na kuuza sera za chama hicho ili kutimiza ajenda ya demokrasia na maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *