Vijana kunufaika na kituo cha ICT kilichozinduliwa eneo bunge la Voi

Eneo bunge la Voi kaunti ya Taita-Taveta limezindua  kituo cha teknolojia ya habari na mawasiliano  kama njia moja ya kuwawezesha vijana kufanya kazi za mtandaoni na pia kuboresha elimu ya dijitali katika eneo hilo.

Mbunge wa Voi Johnes Mlolwa alisema kituo hicho kitawahudumia takribani vijana 5000 katika kaunti hiyo ndogo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho Alhamisi, mbunge huyo alitaja kituo hicho cha teknolojia ya habari na mawasiliano kuwa hatua ya kuhakikisha vijana wanajitegemea kupitia ajira na biashara za mtandaoni.

“Kile tunachofanya ni kuwapa vijana mikakati na rasilimali ili watumie mtandao kujikimu kimaisha,” alisema Mlolwa.

Mbunge huyo alisema kuna mipango ya kushirikiana na wizara ya Teknolojia ya habari na mawasiliano kutengeneza vituo zaidi katika wadi sita za kaunti hiyo ndogo.

Mwakilishi wanawake wa kaunti hiyo Lydia Haika aliyeandamana na mbunge huyo aliwasihi vijana kutumia kikamilifu kituo hicho kujinufaisha.

Alisema ukuaji wa kimtandao unawawezesha vijana kufanya kazi hata wakiwa nyumbani.

“Janga la virusi vya Covid-19 limetufunza kwamba tunaweza fanya kazi tukiwa nyumbani,” alisema Haika.

Alitoa wito wa uwekezaji zaidi katika sekta za vijana ili waimarishe ujuzi wao.

Kituo hicho kiligharimu shilingi bilioni 1.3, kina vipakatalishi 10 na kimeunganishwa kwa mtandao wa kasi ya juu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *