Vifaa vya Zoom ni vyangu!

Msanii wa muziki nchini Tanzania Harmonize mmiliki wa kampuni ya usimamizi wa wasanii maarufu kama Konde Music amedai kwamba yeye ndiye mmiliki halisi wa vifaa vinavyotumika kwenye studio za kutayarisha muziki kwa jina “Zoom Extra” ambayo awali iliitwa “Zoom”.

Konde Boy anasema vifaa hivyo ambavyo hutumika huko Wasafi au ukipenda WCB alikogura ni vyake kwani alifungua studio ya Zoom akiwa bado WCB.

Harmonize alikuwa akihojiwa ambapo alifunguka na kuelezea kwamba alinunua vifaa hivyo nchini Afrika Kusini, na aliporudi akamtafuta Ken the Producer wakaanzisha studio hiyo na baadaye wakaamua kumhusisha Diamond ili asilalamike kwamba anafanya mambo kivyake.

Mwanamuziki huyo anasema kuondoka kwake WCB sio kitu ambacho alipanga na hajawahi kuambia umma kilichomsukuma atoke lakini akaacha Ken kwenye Wasafi wakati huo ndio hiyo studio ilibadilishwa jina ikawa “Zoom Extra”.

Alipohojiwa kwenye kituo cha redio cha Wasafi Fm mwezi Septemba mwaka 2019 Ken alisema kwamba yeye ndiye msimamizi wa Zoom Production hata baada ya Harmonize kusema kwamba Jose wa Mipango ndiye alikuja na wazo la Zoom Production.

Ken alisema pia kwamba Zoom Production iko katikati yaani inafanya kazi na kampuni zingine ambazo zinachagua kufanya kazi nayo.

Watangazaji siku hiyo walisoma wasifu wa Diamond Platnumz kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo ameorodhesha kampuni ambazo aliasisi na anazisimamia na Zoom Extra ni moja yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *