Vanessa Mdee achumbiwa na Rotimi

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Vanessa Mdee amevishwa pete ya uchumba na mpenzi wake ambaye ni mwanamuziki, muigizaji na mwanamitindo wa Marekani Rotimi.

Olorutimi Akinisho, alimvisha mpenzi wake pete hiyo ya uchumba kwenye hafla ya wageni wachache na video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inamwonyesha akiwa amepiga magoti akimuuliza ikiwa atakuwa mke wake.

Vanessa anaonekana kuzidiwa na hisia kisha anasema ndio, anavishwa pete na wanakumbatiana.

Vanessa na Rotimi wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi tangu mwezi Oktoba mwaka 2019.

Mwanadada huyo aliyeacha kazi yake ya muziki ili kutumia muda wake mwingi na mpenzi wake, aliweka video fupi kwenye akaunti yake ya Instagram ikionyesha pete ya thamani aliyovishwa huku akiandika maneno mengi kuhusu mapenzi yao.

Anasema ulimwengu ulimcheka alipokiri kwamba Rotimi ndiye mume wake siku chache baada ya kujuana naye kwani awali alikuwa amesema hakuwa na nia ya kuolewa.

Mipango aliyokuwa nayo wakati akifikisha umri wa miaka 30 anasema ni tofauti na aliko kwa sasa kwani binadamu hupanga na Mungu akapangua. Anataja kifungu cha Biblia cha Yeremia 29:11 ambacho kinasema kwamba Mungu ana mipango mizuri kwa kila mmoja.

Rotimi ambaye huigiza kwenye kipindi kwa jina “Power” naye alipachika video hiyo ya pete aliyomvisha Vanessa akisema aliomba Mungu ampe mke mzuri mwaka 2015 na sasa amempata na ana kila sababu ya kushukuru Mungu.

Sasa kinachosubiriwa ni arusi ya nyota hao wawili ambao wamekuwa wakionyeshamapenzi yao kwenye mitandao ya kijamii. Rotimi alizaliwa New Jersey Marekani lakini wazazi wake wanatokea nchini Nigeria na Vanessa Mdee, alizaliwa katika eneo la Ausha nchini Tanzania lakini kwa sasa wawili hao wanaishi Atlanta, Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *