Uzalishaji Chakula kaunti ya Baringo wapigwa jeki na Benki ya maendeleo Barani Afrika

Uzalishaji wa chakula katika maeneo ya nyanda za chini ya eneo la Kerio katika kaunti ya  Baringo umeimarika kufuatia kuboreshwa kwa mpango wa unyunyuziaji mashamba maji wa Kiboi na benki ya maendeleo barani Afrika kwa ushirikiano na serikali ya taifa.

Kupanuliwa na kukarabatiwa kwa mradi huo ambako kulifadhiliwa kupitia kwa mpango wa kukabiliana na ukame na kudumisha maisha kwa kima cha shilingi milioni  88 kumeshuhudia kuongezeka kwa ekari kutoka mia moja mwaka wa  2013 hadi ekari  400.

Akiongea katika afisi yake mjini  Kabarnet, mshirikishi wa mpango huo  Elphas Ruto, alisema kuwa kazi ya ukarabati imewezesha zaidi ya familia 170  kujihusisha zaidi katika kilimo mseto na kile cha ukuzaji wa mboga na matunda.

Alisema kuwa mradi huo umesambaza mbegu maalum na pembejeo za thamani ya shilingi milioni 4.2 kwa wakulima.

Ruto alielezea matumaini kuwa uzalishaji utaimarika msimu huu baada ya asilimia 80 ya ardhi iliyolimwa kutumika kikamilifu. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *