Categories
Habari

Usalama waimarishwa Pwani huku wageni wakitarajiwa wakati huu wa sherehe

Serikali imeimarisha usalama katika eneo la Pwani huku maelfu ya wageni wakitarajiwa kuzuru eneo hilo wakati huu wa msimu wa sherehe.

Kamishna wa eneo la Pwani John Elungata alisema mikakati yote ya kiusalama iko tayari kuhakikisha wenyeji na hata wageni wanafurahia msimu wa sherehe kwa amani.

“Tuna maafisa wa kutosha wa usalama na pia tumeboresha doria katika fuo zote na katika maeneo maarufu,” alisema Elungata.

Kulingana na Elungata maafisa wote wa usalama pamoja na wazee wa vijiji wamewekwa katika hali ya tahadhari kuhakikisha mazingira salama kwa wageni wa humu nchini na wale wa mataifa ya kigeni.

Wakati huo huo Elungata alitoa wito kwa wamiliki wa sehemu za burudani kuhakikisha sheria za kudhibiti msambao wa virusi vya Covid-19 vinazingatiwa kikamilifu.

“Watakaopatikana wakikiuka sheria za kudhibiti Covid-19 watatiwa nguvuni na kufikishwa mahakamani,” alionya mtawala huyo.

Kwa upande wake kamanda wa polisi katika eneo la Pwani Gabriel Musau aliyeandamana na Elungata, alidokeza kuwa maafisa  500 wa magereza  wanasaidiana na maafisa wengine wa usalama katika msimu huu wa sherehe.

“Tunawakaribisha wakenya na raia wa kigeni Pwani huku tukiwahakikishia usalama wao wakati huu wa msimu wa sherehe,” alisema Musau.

Musau alisema maafisa wa polisi watashirikiana na halmashauri ya uchukuzi na usalama barabarani,NTSA kuhakikisha sheria za trafiki zinafuatiliwa kikamilifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *