Urusi yaimarisha usalama katika eneo la mzozo la Nagorno-Karabagh

Mamia ya walinda usalama wa Urusi wamepelekwa katika eneo linaogombaniwa la Nagorno-Karabagh kufwatia mkataba wa kumaliza mzozo huo.

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea kati ya Azerbaijan na Armenia kwa wiki kadhaa, hadi pande hizo mbili zilipokubali mkataba wa kusitisha mapigano hayo chini ya udhamini wa Urusi siku ya Jumatatu.

Jimbo hilo linatambuliwa kimataifa kuwa sehemu ya Azerbaijan lakini tangu mwaka wa 1994, limekuwa likisimamiwa na wakazi wa asili ya Armenia.

Kuafikiwa kwa mkataba huo kulisababisha furaha miongoni mwa wakazi wa Azerbaijan na hasira katika jimbo hilo la Armenia.

Chini ya mkataba huo, Azerbaijan itamiliki maeneo ambayo ilitwaa wakati wa mapigano ya hivi majuzi.

Armenia ilikubali kuyaondoa majeshi yake kutoka maeneo fulani ya Azerbaijan.

Wataalamu wa maswala ya kisiasa wamesema kuwa mkataba huo ni ushindi kwa Azerbaijan lakini pigo kubwa kwa Armenia.

Waandamanaji nchini Armenia waliharibu sehemu za majengo ya serikali na kumtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo kujiuzulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *