Umoja wa Mataifa wakashifu mauaji ya raia nchini Myanmar

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limekashifu vikali mauaji ya mamia ya raia nchini Myanmar, kwenye taarifa iliyopuuziliwa mbali na China siku mbili baada ya majadiliano kuhusu swala hilo.

Kwenye taarifa , wanachama wa baraza hilo walielezea masikitiko yao kuhusiana na hali ilivyo nchini humo, huku wakipinga kutumiwa kwa nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wakiwemo kina-mama na watoto.

Tangu kupinduliwa kwa serikali ya nchi hiyo tarehe moja mwezi Februari mwaka huu, baraza hilo la umoja wa mataifa, limekuwa likitoa taarifa yake kwa mara ya tatu sasa.

Lakini China, ambayo haijawahi kukubali kuwepo kwa mapinduzi nchini Myanmar, imesababisha kujikokota kwa mazungumzo kusitisha mauaji hayo.

Mbali na hayo, msimamo wa baraza hilo haujasababisha kuchukuliwa kwa hatua yoyote dhidi ya mauaji hayo.

Siku ya Jumatano, balozi wa umoja wa mataifa nchini Myanmar, alitaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya serikali hiyo ya kijeshi.

Kwa mujibu wa balozi huyo, jinsi hali ilivyo nchini humo, huenda kukazuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Msimamo wa baraza hilo unajiri wakati ambapo kiongozi aliyeng’olewa mamlakani Aung San Suu Kyi akiongezewa shtaka lingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *