Categories
Habari

Umaskini watajwa chanzo cha dhuluma za kijinsia

Serikali imezindua mipango ya kuwapa uwezo wanawake kwa lengo la kukabiliana na visa vya dhuluma za kijinsia ambavyo vimekithiri hapa nchini.

Waziri wa utumishi wa umma na jinsia Prof. Margret Kobia ametaja umaskini kuwa suala linalochangia visa vya dhuluma za kijinsia kwa kiwango kikubwa zaidi huku wanawake wakiathirika kuliko wanaume.

Prof. Kobia ambaye alitoa hundi za thamani ya shilingi milioni 25.7 kwa makundi  87 ya wanawake katika kaunti ya  Embu, aidha alisema hazina ya kufadhili biashara za wanawake itaimarishwa kwa kuanzisha aina mpya za mikopo ili kuhimiza wanawake kukopa pesa kutoka hazina hiyo.

Alisema pia kuwa hazina hiyo itaboresha uwezo wa makundi hayo ya wanawake wa kukopa pesa hizo kutoka shilingi  750, 000 hadi shilingi milioni moja licha ya kuanzisha mpango wa ufadhili wa mali ambapo wanachama wanaweza kukopa ili kununua mali wakiwa kwenye kundi au mtu binafsi.

Kulingana na Prof. Kobia, takwimu zinaashiria kuwa asilimia  90 ya wanawake wameathirika kutokana na visa vya dhuluma za kijinsia ikilinganishwa na asilimia 10 ya wanaume.

Kamishna wa kaunti ya Embu Abdulahi Galgalo, amewataka wazazi , viongozi wa kidini na maafisa wa utawala kushirikiana kukabiliana na uovu huo ambao unaendelea kutishia udhabiti wa familia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *