Ulinzi Stars waiangusha Mathare United huku Gor wakiiparuza Zoo Fc ligi kuu FKF

Wanajeshi Ulinzi Stars  na mabingwa watetezi Gor Mahia wamesajili ushindi katika mechi mbili za ligi kuu FKF  zilizosakatwa Jumatano alasiri.

Ulinzi waliipakata Mathare United mabao  2-1 katika uwanja wa Afraha  ,Daniel Waweru akipachika bao la kwanza kwa wenyeji kunako dakika ya 7 akiunganisha mkwaju uliotumwa na Michael Otieno na kumwacha kipa hoi bin taaban.

Kiungo Elvis Nandwa aliongeza bao la pili kwa Ulinzi akiunganisha pasi  murua iliyochongwa na mchezaji Masuta katika dakika ya 70 huku Mathare wakijipatia goli la maliwazo kupitia kwa Daniel Otieno dakika ya 88.

Katika mechi nyingine iliyopigwa katika uchanjaa wa Kasarani, Gor Mahia walirejelea tambo za ushindi na kuititiga Zoo Fc mabao 3 bila jibu ,kiungo Samuel Onyango akipachika la kwanza dakika ya 10, kabla ya nahodha Keneth Muguna kutanua uongozi kwa goli la dakika ya 32 na kisha Onyango akapiga tena bao la tatu kunako dakika ya pili ya muda wa mazidadi.

Kufuatia matokeo ya Jumatano Gor na Ulinzi wamezoa idadi sawa ya alama 12 ingawa vijana wa KDF wamecheza mechi mbili zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *