Ukusanyaji saini za BBI kuanza rasmi leo

Uzinduzi wa zoezi la kukusanya saini kwa ajili ya mswada wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI, unatarajiwa kufanyika leo.

Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wanatarajiwa kuongoza hafla ya uzinduzi huo itakayofanyika katika Ukumbi wa KICC, Jijini Nairobi.

Mapema wiki hii, kamati ya kitaifa ya BBI ilitangaza kwamba mswaada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020 uko tayari na kinachotakiwa kufuata ni shughuli hiyo ya ukusanyaji saini.

Kamati hiyo inawahimiza wanaounga mkono mchakato wa BBI kujitokeza kwa wingi ili kuweka saini zao katika muda wa wiki moja ambao zoezi hilo litafanyika.

Shughuli hiyo iliahirishwa wiki iliyopita kutokana na kucheleweshwa kwa uchapishaji wa mswaada huo wa marekebisho ya katiba.

Kinara wa ODM Raila Odinga alikutana na viongozi wawili wa kamati ya BBI, Dennis Waweru na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed kwa ajili ya matayarisho ya hafla ya leo.

Baada ya shughuli ya ukusanyaji saini kukamilika, kamati hiyo itazipeleka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kwa uthibitisho.

Baadaye mswaada huo wa marekebisho ya katiba utapelekwa katika Mabunge yote ya Kaunti nchni ili kujadiliwa.

Ikiwa zaidi ya nusu ya mabunge hayo yataupitisha, mswaada huo utapelekwa kwa Bunge la Kitaifa kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa kabla kura ya maamuzi kuandaliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *