Uhusiano kati ya Kenya na Ethiopia kuimarishwa huku Kituo cha Mpakani cha Moyale kikizinduliwa

Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wameahidi kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na Ethiopia katika juhudi za kuleta maendeleo katika eneo hilo.

Viongozi hao wameahidi hayo walipokuwa wakifungua rasmi kituo kimoja cha huduma cha mpakani huko Moyale katika Kaunti ya Marsabit.

Rais Kenyatta alikuwa amemlaki Waziri Mkuu wa Ethiopia huko Marsabit mwanzoni mwa ziara rasmi ya siku mbili ya kiongozi huyo humu nchini.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, Rais amesema kuwa kituo hicho kitarahisisha uhamiaji na huduma za forodhani baina ya nchi hizo mbili na pia kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya chumi hizi mbili kuu za kanda ya Afrika Mashariki.

“Ninashawishika kwamba kungali na nafasi kubwa ya kukuza biashara na pia ninatambua umuhimu wa ushirika na uendelezaji wa miradi ya miundombinu ya pamoja ambayo itazidi kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya Kenya na Ethiopia,” akasema Rais Kenyatta.

Kenya na Ethiopia zilitia saini mkataba mwaka wa 2011 kuanzisha kituo kimoja cha huduma cha mpakani pamoja na barabara ili kuboresha uhusiano wa kibiashara.

Rais Kenyatta na Abiy watakagua ujenzi unaoendelea wa Bandari ya Lamu ambao ni sehemu ya barabara kutoka bandari ya Lamu-Sudan Kusini hadi Ethiopia, (Lapsset).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *