Uhuru aongeza muda wa kafyu huku akitarajiwa kuhutubia taifa wiki ijayo

Muda wa utekelezaji wa kanuni zilizopo za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19 umeongezwa hadi Jumanne wiki ijayo ambapo Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuhutubia taifa.

Hotuba hiyo ya rais ya kumi na mbili kuhusu janga la COVID-19 imewadia wakati ambapo nchi hii imeshuhudia kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo, hali ambayo huenda ikaashiria utayari wa kufunguliwa kwa uchumi na taasisi za masomo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, Rais Kenyatta atatoa mwelekeo mpya wa taifa hili kuhusu janga hilo juma lijalo tarehe 29.

Jumatatu tarehe 28, Rais Kenyatta anatarajiwa kuongoza kikao cha Kamati ya kitaifa ya kukabiliana na virusi vya corona NERC chenye lengo la kutoa mwelekeo zaidi kabla rais kutoa hotuba yake siku itakayofuata.

“Hotuba hiyo ya Kiongozi wa Taifa itatoa kanuni mpya zitakazoongoza nchi hii katika ukawaida mpya. Hivyo basi mnaelezwa kuwa rais ameongeza muda wa utekelezaji wa kanuni zilizotangazwa wakati wa hotuba ya 11 ya rais hadi Jumanne tarehe 29 Septemba, 2020,” ameeleza.

Hotuba hiyo inatarajiwa kutoa mwongozo kwa Wakenya wa jinsi ya kuishi kwenye janga la COVID-19, na jinsi ya kujikwamua kutokana na kudorora kwa uchumi.

“Itadhihirisha hatua za kuimarisha uthabithi wa kiuchumi na kujitegemea, ikiwemo kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa nchi hii,” ameongeza Kinyua.

Watu kadhaa ambao wamedhihirisha kuwa ‘Mashujaa wa COVID-19’ kwa juhudi zao za ukarimu wa kutoa huduma katika kusaidia Kenya kwenye vita dhidi ya janga hilo watatambulia siku hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *