Uholanzi yasitisha kwa muda utumizi wa chanjo ya Oxford-AstraZeneca

Uholanzi imesitisha utoaji wa chanjo ya Oxford-AstraZeneca dhidi ya COVID-19 hadi tarehe 7 mwezi huu.

Siku ya Ijumaa wizara ya afya nchini humo ilisema kuwa itasitisha kwa muda utoaji chanjo kwa watu walio na umri wa chini ya miaka 60.

Hata hivyo baada ya mashauriano Jumamosi, idara za afya ziliamua kusitisha utoaji chanjo ya aina hiyo ili kuepusha uharibifu.

Watu 700 walio na umri wa zaidi ya miaka 60 walifaa kupokea chanjo ya AstraZeneca katika siku zijazo lakini utoaji huo wa chanjo ukafutiliwa mbali kwa muda kwani hakukuwa na ithibati kwamba shehena kamili itatumiwa yote iwapo ni watu wachache tu watakaopokea chanjo hiyo.

Uamuzi huo umejiri siku chache baada ya maafisa nchini Ujerumani pia kusitisha utoaji chanjo ya AstraZeneca kwa watu wa umri wa chini ya miaka 60,wakiibua wasiwasi kuhusu kuganda kwa damu miongoni mwa watu wachache waliopata chanjo hiyo.

Waziri wa afya Hugo de Jonge, alisema kuwa kusitishwa kwa muda kwa utoaji wa chanjo hiyo ni hatua ya tahadhari.

Uamuzi huo ulioafikiwa Jumamosi, ni pigo jingine kwa chanjo hiyo ya AstraZeneca ambayo ni muhimu kwa kampeni ya bara ulaya ya kutoa chanjo na pia ni muhimu kwa mikakati ya kimataifa ya kuwasilisha chanjo kwa nchi maskini kwani ni ya bei nafuu na ni rahisi kutumia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *