Ugavana wa Okoth Obado wayumba

Hatma ya Okoth Obado kama gavana wa kaunti ya Migori haibainiki baada ya mkutano wa wajumbe wa chama cha ODM kuazimia kwa kauli moja kwamba aondolewe kwenye wadhifa huo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi, wajumbe hao walisema Obado hafai kuendelea kuhudumu kama gavana wa Migori baada ya kushtakiwa Pamoja na wanawe kuhusiana na ufujaji wa pesa za kaunti hiyo.

Mbadi alisema hoja ya kumuondoa mamlakani gavana Obado iliyopangiwa wiki ijayo imeidhinishwa na kiongozi wa chama hicho Raila Odinga.

Mbadi aliyeandamana na seneta wa kaunti hiyo Ochillo Ayako na viongozi wengine alisema chama cha ODM hakitawavumilia viongozi wafisadi haswa wale wanaoshikilia nyadhifa muhimu.

Badi alipuzilia mbali madai kuwa chama hicho kinamyanyasa Obado akisema hakuna gavana mwingine aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama hicho aliyeshtakiwa kwa ubadhirifu wa pesa kiasi hicho wala kuagizwa kutofika afisini mwake na mahakama.

Hayo yamejiri huku spika wa kaunti hiyo akiandikisha taarifa kwa maafisa wa polisi akidai Maisha yake yamo hatarini kufuatia mpango huo wa hoja ya kumuondoa Obado mamlakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *