Categories
Kimataifa

Uganda yakana madai kwamba viongozi wakuu serikalini wamechanjwa kisiri dhidi ya COVID-19

Waziri wa Afya nchini Uganda Jane Aceng amekanusha taarifa kwamba viongozi wa juu wa serikali wamepata chanjo dhidi ya COVID-19 hata kabla ya taifa hilo kupokea rasmi chanjo hizo.

Kwenye ujumbe wa Twitter, Aceng amesema rais na wandani wake wa karibu hawajapokea chanjo hizo jinsi ilivyodaiwa.

Uganda inatarajiwa kupokea dozi laki moja za chanjo kutoka kampuni ya India, AstraZeneca na nyingine 300,000 kutoka kampuni ya Sinopharm ya Uchina.

Hata hivyo, haijathibitishwa ikiwa chanjo hizo zimewasili katika taifa hilo ambalo kufikia sasa limethibitisha visa 40,221 vya COVID-19.

Kumekuwa na mgogoro katika usambazaji wa chanjo hizo duniani, huku Rais wa Rwanda Paul Kagame akikerwa na unafiki na hujuma kwenye usambazaji wa chanjo hizo hasa kwa mataifa yenye kipato cha chini.

Rais Kagame alisema hayo kwenye ujumbe wake baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus kusema kuwa makubaliano kati ya nchi tajiri na watengenezaji wa chanjo hizo yametatiza ununuzi na usambazaji wa chanjo hizo kupitia mpango wa Covax.

Mpango wa Covax unanuia kuhakikisha usawa katika usambazaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 miongoni mwa mataifa yote duniani.

Mnamo mwezi Disemba, vuguvugu la People’s Vaccine Alliance lilionya kwamba asilimia 70 ya mataifa ya kipato cha chini yataweza kutoa chanjo kwa asilimia kumi pekee ya raia wake.

Lilitoa wito kwa kampuni zinazotengeneza chanjo hizo kutoa habari kuhusu teknolojia inayotumika ili kurahisisha utengenezaji na kuwawezesha watu wengi zaidi kupata chanjo hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *