Uganda Hippos wabanwa mbavu na Sudan Kusini CECAFA

Uganda walilazimishwa kwenda sare tasa dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya ufunguzi ya kundi B kuwania kombe la Cecafa kwa vijana walio chini ya umri wa  miaka 20 iliyochezwa Jumatatu jioni katika uwanja wa Black Rhino Academy Complex.

Ilikuwa mara ya  tatau mtawalia kwa timu ya Uganda kutatizwa na  Sudan Kusini,baada ya Uganda Cranes kuhitaji bao la dakika ya mwisho kabla ya kuishinda Sudan Kusini katika pambano  kufuzu kwa kombe la Afcon jijini Kampala kabla ya kucharazwa na Sudan Kusini bao 1-0 kwenye mechi ya marudio iliyochezwa katika uwanja wa taifa wa Nyayo.

Uganda maarufu kama Hippos  watarejea uwanjani Jumatano kwa mechi ya pili dhidi ya Burundi mechi ambayo lazima washinde ili kufuzu kwa nusu fainali.

Mashindano ya Cecafa yataingia siku ya tatu Jumanne kwa mchuano mmoja wa kundi  A kati ya Djibouti na Somalia katika uwanja wa Black Rhino Academy Complex kuanzia saa kumi alasiri.

Mechi za makundi zitafikia tamati Ijumaa kabla ya nusu fainali kung’oa nanga Novemba 30 ikifuatwa na fainali ya Disemba 2.

Timu bora kutoka kila kundi na timu bora ya pili kutoka makundi yote matatu zitafuzu kwa nusu fainali ilihali timu mbili bora zikifuzu kuwakilisha ukanda wa Cecafa katika mashindano ya kombe la mataifa ya afrika Afcon mwaka ujao nchini Mauritania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *