Ufaransa kulegeza masharti ya COVID-19 msimu wa Krismasi

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema nchi yake itaanza kulegeza masharti yaliyowekwa katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Corona, kwa kuruhusu baadhi ya maduka kuendelea na biashara zao, kuanzia mwishoni mwa juma hili.

Macron ametangaza kuwa watu wataruhusiwa pia kutangamana na familia zao msimu ujao wa sherehe za Krismasi.

Hata hivyo, rais huyo amesema baa na migahawa zitaendelea kufungwa hadi tarehe 20 Januari mwaka ujao.

Ufaransa imeripoti zaidi ya visa milioni 2.2 vya watu walioambukizwa Corona na vifo vya zaidi ya watu elfu 50 tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza cha ugonjwa wa COVID-19 nchini humo.

Kupitia hotuba ya televisheni, Macron amesema nchi yake imepita kilele cha wimbi la pili la maambukizi ya Corona.

Amesema kwamba masharti mengi yaliyotangazwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo yatalegezwa kaunzia tarehe 15 Desemba kwa ajili ya sherehe za Krismasi, ambapo kumbi za sinema zitafunguliwa na masharti yaliyowekewa shughuli za usafiri kuondolewa iwapo kiwango cha maambukizi mapya kitakuwa chini ya visa 5,000 kwa siku.

Mnamo siku ya Jumatatu, Ufaransa ilitangaza visa vya watu 4,452 walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 katika muda wa masaa 24, hiyo ikiwa idadi ya chini zaidi nchini humo tangu tarehe 28 Septemba.

Kiwango cha wastani cha maambukizi ya Corona kwa siku kilikuwa visa 21,918 ambapo kilele chake kilikuwa visa 54,440 mnamo tarehe 7 mwezi huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *