UDA chamteua Urbanus Muthama Ngengele kuwania Useneta wa Machakos

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kimemteua mfanyibiashara Urbanus Muthama Ngengele kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo wa kiti cha useneta cha Machakos.

Kaimu mwenyekiti wa chama hicho Johnstone Muthama alisema uteuzi huo ulitokana na kura ya maoni iliyofanyiwa umaarufu wa mwaniaji huyo.

Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Seneta Boniface Kabaka tarehe 11 mwezi Disemba mwaka jana baada ya kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Nairobi hospital.

Wawaniaji wengine katika kinyang’anyiro hicho ni pamoja na Agnes Kavindu, ambaye ni mke wa zamani wa aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama, atakayewania kwa tikiti ya chama cha Wiper Democratic Movement.

Waziri wa zamani Mutua Katuku pia atawania wadhifa huo kwa tikiti ya chama cha Maendeleo Chap Chap.

Chama cha Jubilee kimedinda kuweka mwaniaji katika uchaguzi huo mdogo.

Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju aliwaambia wanahabari siku ya Jumatano kwamba  chama hicho kiliazimia kutoshiriki katika uchaguzi huo mdogo.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ilibadilisha tarehe ya uchaguzi huo mdogo kutoka tarehe 23 mwezi Machi mwaka huu hadi tarehe 18 mwezi huo huo wa Machi baada ya wizara ya elimu kuarifu IEBC kuwa tarehe ya awali iliwiana na mitihani ya kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *