Uchunguzi waanzishwa kuhusu ajali ya helikopta Narok

Halmashauri ya Uchukuzi wa Ndege nchini KCAA imeanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali ya ndege aina ya helikopta iliyotokea katika kaunti ya Narok.

Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo Nahodha Gilbert Kibe, kwenye taarifa, amesema kuwa idara ya uchunguzi wa ajali za ndege tayari imeanzisha uchunguzi, na itawafahamisha wananchi mara tu itakapokamilisha.

Gavana wa Narok Samuel Tunai na watu wengine watatu hapo jana walinusurika kwenye ajali hiyo katika eneo la Eldamat.

Tunai alikuwa akiondoka kwenye hafla ya mazishi ya Tompo Ole Sai, kisa hicho kilipotokea.

Wale walioshuhudia kisa hicho wanasema kuwa rubani wa helikopta hiyo yenye nambari ya usajili 5YMEP, aina ya Robinson 44 alijaribu kupaa mara kadhaa lakini akashindwa.

Inadaiwa kuwa baada ya kupaa kwa mara ya tano, ndege hiyo ilianguka baada ya kwenda umbali wa mita 100 tu.

Tunai na wengine waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini kwa ambalanzi ya Shirika la Msalaba Mwekundu.

Mwakilishi wa Wadi ya eneo hilo Moses Ole Samante, alisema kuwa gavana yuko salama kiafya na hakuna sababu yoyote ya kuhofu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *