Uchunguzi wa nyama wabainisha kuwepo kwa viini vya magonjwa

Uchunguzi wa hivi majuzi wa nyama ya nguruwe na kuku inayouzwa katika kaunti za Nairobi, Kisumu, Nakuru, Laikipia, Uasin Gishu na Nyeri umebainisha kwamba bidhaa hizo zimesheheni viini vya magonjwa.

Uchunguzi huo ulifanywa na shirika la utunzi wa wanyama ulimwenguni kati ya mwezi Aprili na Julai mwaka jana, na kushirikisha sampuli 187 za nyama ya nguruwe na sampuli 206 za bidhaa za kuku kutoka maduka ya rejareja kwenye kaunti hizo husika.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, asilimia 98.4 ya sampuli za bidhaa za nguruwe ilikuwa na viini vya magonjwa ilhali asilimia 96.6 ya sampuli 199 za bidhaa za kuku pia ilikuwa na viini.

Daktari Victor Yamo kutoka shirika hilo, alisema hali hiyo imesababishwa na utumizi mbaya wa dawa za nguruwe na kuku kutokana na ukosefu wa usimamizi mwafaka wa mashamba wanamofugwa.

Dkt. Yamo alisema asilimia 70 ya dawa zinazopewa nguruwe, kuku na ng’ombe humu nchini huagizwa kutoka mataifa ya nje.

Daktari huyo alitoa wito kwa serikali kuchukua hatua na kubuni sera madhubuti kulainisha matumizi ya dawa miongoni mwa mifugo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *