Uchanjaa wa Al Rayyan wakamilika kwa kipute cha kombe la dunia Qatar
Kamati andalizi ya fainali za kombe la dunia mwaka 2022 nchini Qatar imetangaza kukamilishwa kwa ujenzi kwa uwanja wa Al Rayyan tayari kwa kipute hicho.
Kwa mjibu wa kamati hiyo hafla ya kuufungua rasmi uchanjaa huo itakuwa tarehe 18 mwezi huu ambayo ni siku ya kitaifa nchini Qatar huku ikiadhimisha miaka miwili kabla ya mechi ya fainali ya kombe la dunia itakayoandaliwa Disemba 18 mwaka 2022.
Uwanja huo utakuwa wa nne kukamilika tayari ya kipute hicho na utakuwa uwanja mpya wa kilabu cha Al Rayyan Sports Club na unajiunga na viwanja vingine vitatu vilivyokamilika vikiwa ni :- Khalifa International, Al Janoub na Education City.
Kiwara cha Al Rayyan kilicho na uwezo wa kuwaselehi mashabiki wapatao 40,000 kimeratibiwa kutumika kuandaa mechi 7 hadi raundi ya 16 bora wakati wa fainali hizo za kombe la dunia .