Tume ya TSC kuwaajiri walimu 6,674 wa muda

Tume ya TSC imetangaza nafasi za kazi za walimu wa muda 6,674  watakaohudumu katika shule za msingi na upili.

Walimu hao watasaidia kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi madarasani.

Kwenye tangazo lake katika magazeti ya humu nchini, tume hiyo imesema walimu-1,998 watapelekwa katika shule za msingi ilihali-4,676 watafunza katika shule za upili.

Kulingana na tangazo hilo kuajiriwa kwa walimu hao ni mojawapo wa mpango wa kufufua uchumi uliotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kwenye  hotuba yake ya saba kwa taifa kuhusu janga la Covid-19.

Watakaopelekwa katika shule za msingi watalipwa  shilingi alfu 15 kwa mwezi ilhali wale wa shule za upili watalipwa shilingi alfu 20 kila mwezi.

Walimu hao watahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja na watatunukiwa vyeti mwishoni mwa kipindi hicho.

Ili kufuzu kwa ajira hiyo, mtahiniwa sharti awe Mkenya halisi, awe na Stashahada ya elimu na awe amesajiliwa na tume ya TSC.

Kwenye mipango ya ufunguzi wa shule, TSC imesema itatoa mafunzo kuhusu mtaala mpya wa elimu CBC kwa walimu 118,000 kwa gharama ya shilingi bilioni  moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *