Tume ya kudhibiti kawi nchini yatangaza bei mpya ya bidhaa za petroli

Bei ya mafuta ya petrol ya  Super imeongezeka kwa shilingi moja na senti 48 katika mabadiliko ya hivi punde yaliyotangazwa na tume ya kudhibiti kawi na mafuta.

Katika mabadiliko hayo bei ya mafuta ya diseli na mafuta taa ilipungua kwa senti 12 na senti hamsini mtawalia kwa lita

Bei hizo zinajumuisha asilimia nane ya ushuru ziada wa thamani kuambatana na sheria ya kifedha ya mwaka wa 2018 na sheria za ushuru.

Halmashauri hiyo ilisema kuwa mabadiliko hayo katika bei za mwezi huu yametokana na gharama za uagizaji wa mafuta ya petrol aina ya Super ambayo iliongezeka kwa asilimia  2.65 kutoka dola  319 na senti 23 za kimarekani kwa pipa mwezi Julai hadi dola 327 na senti 69 mwezi Agosti.

Bei hizo mpya zitaanza kutekelezwa tarehe 15 mwezi Septemba hadi tarehe 14 mwezi Octoba.

Jijini  Nairobi, mafuta ya  Petroli ya Super yatakuwa yakiuzwa kwa shilingi  105 na senti 43 kwa lita huku yale ya diesel yakiuzwa kwa shilingi  94 na senti 51 kwa lita.

Mafuta taa yatakuwa yakiuzwa shilingi  83 na senti 15 kwa lita.

Huko Mombasa, mafuta ya petroli ya super  yatauzwa kwa shilingi 103 na senti 5 kwa lita, mafuta ya diseli yauzwe kwa shilingi  92 na senti 15 kwa lita huku mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi  80 na senti 78 kwa lita.

Bei za mafuta ya petrol na  diseli ziliongezeka kwa shilingi 11 na senti 38 na shilingi 17 na senti 30 mtawalia katika mabadiliko yaliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *