Tume ya IEBC yatangaza nafasi 400 za ajira

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imetangaza nafasi za kazi kwa makarani watakaothibitisha saini zilizokusanywa kuhusu mchakato wa maridhiano ya kitaifa, BBI.

Katika tangazo hilo, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema makarani hao 400 ambao wataajiriwa kwa muda watalipwa shilingi 1,200 kwa siku.

“Watakaotuma maombi ni sharti wawe raia wa Kenya, wana vyeti vya mtihani wa kidato cha nne, wanaujuzi wa kutumia tarakilishi, wana ujuzi wa takwimu na watapatikana katika kipindi hicho cha kuidhinisha sahihi hizo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kulingana na taarifa, hiyo maombi ya nafasi hizo yatatumwa kupitia kwa mtandao na mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 24 mwezi huu wa Disemba.

Tarehe 10 mwezi Disemba mwaka huu, tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, ilipokea mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020 pamoja na sahihi milioni 4.4 kutoka kwa wanaounga mkono mchakato huo.

IEBC kisha iliwasilisha bajeti ya shilingi milioni 241 ili kuwapa makazi ya muda makarani wa zoezi la kuthibitisha saini hizo.

Kulingana na IEBC kuwapa makarani hao makazi ya muda kulikusudia kuwazuia dhidi ya hatari ya kuambukizwa virusi vya Covid-19 kupitia uchukuzi wa umma na pia kutii kafyu iliyoko kwa sasa.

Baadaye IEBC iliwasilisha bajeti ya shilingi milioni 93 na ambayo iliidhinishwa na hazina kuu ya kitaifa.

Bajeti hiyo ni ya makarani ambao hawapewi makazi ya muda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *