Tshala Muana akamatwa na baadaye kuachiliwa

Mwanamuziki wa nchi ya Congo Mama Tshala Muana alikamatwa jumatatu mchana mjini Kinshasa nchini Congo.

Duru zinaarifu kwamba Malkia huyo wa Mutuashi alitiwa mbaroni kutokana na wimbo ambao alirekodi na kuuzindua kwa jina “Ingratitude” maanake kutokuwa na shukrani. Alizindua wimbo huo wiki jana na tangu wakati huo, umekuwa ukizungumziwa sana nchini Congo.

Maneno ya wimbo huo yanasemekana kumlenga Rais wa sasa wa nchi ya Congo Felix Tshisekedi kwa kile ambacho kinasemekana kumgeukia mwandani wake Rais wa zamani wa nchi hiyo Joseph Kabila ingawaje hakuna majina ambayo yametajwa.

Mtayarishaji wa Tshala Muana wa muziki kwa jina Claude Mashala alielezea kwamba maafisa kutoka kitengo cha “National Intelligence Agency, ANR, walimkamata kama mhalifu bila kuheshimu umri wake na kujali afya yake.

Hivi maajuzi kulisambazwa picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha Mama Tshala Muana akiwa anaugua hospitalini.

Inasemekana kwamba Kabila alimsaidia Tshisekedi kuunda serikali ya muungano hata kama muungano huo haujakuwa ukifanya vyema.

Tshala Muana wa umri wa miaka 62 sasa, ni rafiki ya Kabila na alikuwa pia akipigia debe chama chake cha People’s Party for Reconstruction and Democracy,PPRD.

Uhusiano wao unaonekana kujengwa na hatua ya babake Joseph Kabila, Laurent Kabila ya kumteua Tshala Muana kama mbunge wakati akiwa mamlakani.

Kukamatwa kwa mwimbaji huyo wa kibao maarufu ‘Nasi Nabali’ kulisababisha wanawake kadhaa kuandamana katika barabara za mji wa Kinshasa wakitaka aachiliwe huru.

Mama huyo ambaye ni kiungo muhimi katika muziki wa nchi ya Congo aliachiliwa jana jumanne baada ya chama chake cha PPRD kufanya kila juhudi kuhakikisha uhuru wake.

Tshala Muana akiwa amezingirwa na wafuasi wake muda mfupi baada ya kuachiliwa huru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *