Categories
Kimataifa

Trump aondoka katika Ikulu ya Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ameondoka katika Ikulu ya Marekani akiwa ameandamana na mkewe Melania Trump saa chache kabla ya kuapishwa kwa Rais mteule Joe Biden.

Rais huyo na mkewe walielekea katika kambi ya kijeshi iliyoko Maryland ambapo sherehe za mwisho za kuwaaga zilipangiwa kuandaliwa.

Hata hivyo makamu wa Rais, Mike Pence hatahudhuria sherehe za kumuaga Trump lakini anatarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Biden na Harris baadae Jumatano.

Rais Trump akiwahutubia wafuasi wake aliwatakia mafanikio Rais mteule Joe Biden na makamu wake Kamala Harris licha ya kuwa hakuwataja wawili hao kwa majina.

Alisema akiwa katika ikulu ya Marekani aliafikia mengi licha ya janga la Covid-19 kuathiri kipindi cha miezi tisa iliyopita cha utawala wake

Vifo vilivyotokana na Covid-19 nchini humo sasa ni zaidi ya 400,000, na idadi ya vifo imeendelea kuongezeka.

Rais Mteule Joe Biden na makamu wake Kamala Harris wanatarajiwa kuapishwa baadaye Jumatano katika hafla itakayoongozwa na jaji mkuu John Roberts.

Sherehe ya kuapishwa kwa Biden itahudhuriwa na marais wa zamani Barack Obama,Bill Clinton na George W Bush.

Biden atakuwa rais wa Marekani wa 46.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *