Timu ya Kenya kuelekea Dubai kuwania kufuzu kwa Olimpiki ya Walemavu yateuliwa

Majaribio ya kitaifa kuchagua kikosi kitakachoelekea Dubai mwezi ujao kushiriki  uteuzi wa michezo ya Olimpiki kwa walemavu yaliandaliwa Jumatatu katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani  huku vigogo kadhaa wakibwagwa na chipukizi.

Bingwa wa Olimpiki katika mita 5000 T11 mwaka 2016  Samwel Muchai alionyeshwa kivumbi na mshindi wa nishani ya shaba Wilson Bii aliyeibuka mshindi .

Bii alitwaa ushindi kwa dakika  15 sekunde  55 nukta 5 akifuatwa na Muchai anayeuguza jeraha kwa dakika 15 sekunde 56 nukta 3 huku   Rogers Kiprop akiambulia nafasi ya tatu kwa dakika  16 sekunde  12 nukta 5.

Wesley Sang aliibuka mshindi wa mbio za mita 1500 T 46  kwa kusajili dakika  4  na sekunde 2 akifuatwa na Stanley Masik kwa dakika 4 na sekunde 10 huku  Felix Kipruto akiridhia nafasi ya tatu kwa dakika 4  na sekeunde21 nukta 5 .

Mashindano ya riadha ya Dubai  Para Grand Prix  yataandaliwa baina ya tarehe 7 na 14 mwezi ujao yakiwa mojawapo wa mashindano ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki ambayo kamati ya Olimpiki kwa walemavu nchini KNPC  imepanga kuwatuma wanariadha kushiriki.

Mashindano ya Dubai yatafuatwa na yale ya  Tunisia Grand Prix baina ya Machi 18 na 20 , France Grand Prix kati ya  Mei  5 na 7, Morocco Grand Prix mwezi Juni na hatimaye yale ya Mancherster ya kufuzu kwa mchezo wa Powerlifting yatakayoandaliwa mwezi wa tatu mwaka huu.

Kamati ya Olimpiki kwa walemavu nchini KNPC inahitaji jumla ya shilingi milioni 7 nukta 6 kuwatuma wanariadha 30 wasaidizi 8 na maafisa 12 kw amichezo hiyo ya Dubai mwezi Ujao huku Rais wa Kamati hiyo Agnes Aluoch akiiomba serikali kuwasaidia kifedha ili kufanikisha ziara hiyo.

“Tunalenga kuiweka timu katika kambi kuanzia Jumatatu ijayo lakini tunaiomba serikali kutusaidia na shilingi milioni 7 nukta 6 zinazohitajika ili  timu hii iende Dubai bila tashwishwi”akasema Aluoch.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *