“The Letter” kuanza kuonyeshwa nchini

Filamu ya Kenya kwa jina “The Letter” ambayo iliteuliwa kuwania tuzo za awamu ya 93 za Oscar itaanza kuonyeshwa katika kumbi za filamu nchini Kenya kesho tarehe 11 mwezi Disemba mwaka 2020.

Maonyesho hayo yanaambatana na masharti ya tuzo za Oscar kwamba filamu ambayo inateuliwa kuwania tuzo la filamu bora ya kimataifa ionyeshwe katika nchi yake kabla ya tuzo zenyewe.

Ili kutimiza hilo, filamu hito itaonyeshwa kwenye kumbi za Unseen, Anga Diamond, Century Cinemax,Prestige, Motion Cinemas na West Gate Cinemas ambazo zote ziko Nairobi.

Mjini Kisumu, “The Letter” itaonyeshwa katika ukumbi wa Mega Cinemas, mjini Eldoret ionyeshwe ukumbini Rupas na huko Mombasa kwenye ukumbi wa Nyali Cinemax.

Filamu hiyo inaangazia utata unaoghubika umiliki wa Ardhi na inagusa wakenya wengi lakini imeandaliwa katika eneo la Pwani.

Kwa muda mrefu huko Pwani, wakongwe wamekuwa wakisingiziwa kuwa wachawi na kusababisha wengi wao kuuawa.

Lakini inadhihirika wazi kwamba kiini ni umiliki wa ardhi za wakongwe, wanauawa na watu hasa wa familia zao ambao wanataka kumiliki ardhi hizo. Karisa anasafiri kutoka mjini hadi kijijini kufanya utafiti kuhusu barua ya kutishia maisha ya nyayake wa miaka 95.

Baadaye anagundua aliyeandika barua hiyo na anajaribu kukomesha mzozo wa ardhi kati ya mashangazi na wajombake.

Nyanyake pia anaonekana kuwa mjasiri katika mzozo huo kuhusu ardhi.

Muziki ambao umetumika kwenye filamu hiyo, uliandaliwa na mwanamuziki kwa jina Maia Lekow ambaye pia ni mwelekezi msaidizi wa filamu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *