Tanzania yasajili ushindi wa kwanza CHAN na kuitimua Namibia

Taifa Stars ya Tanzania ilisajili ushindi wa kwanza katika michuano ya CHAN inayoendelea baada ya kuwaangusha Namibia goli 1-0 katika mechi ya kundi D iliyochezwa Jumamosi usiku katika uwanja wa Limbe.

Farid Mussa ambaye pia alitawazwa mchezaji bora alifunga bao hilo katika dakika ya 65 alitumia makosa ya mabeki wa Namibia walioshindwa kuondosha mpira katika lango lao na kufyatua mkwaju ulimwacha hoi kipa wa Namibia Kamaijanda Ndisiro.

Namibia maarufu kama Brave warriors walijaribu kwa udi na uvumba kurejesha bao hilo bila mafanikio huku kipa wa Taifa Stars Aishi Manula akipangua mikwaju mingi ya Wanamibia.

Matokeo hayo yanafufua matumaini ya Tanzania kufuzu kwa robo fainali wakihitaji ushindi dhidi ya Guinea Jumatano ijayo ili kufuzu kwa robo fainali.

Katika mechi ya awalia ya kundi hilo Jumamosi jioni Zambia walihitaji bao la dakika ya 87 ili kujinusuru na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Guinea na kuacha kundi hilo wazi kwa nafasi ya kutinga robo fainali.

Victor Kantabadouno aliwaweka Guinea kifua  mbele kwa bao la dakika ya 58  kabla ya Spencer Sautu kusawazishia Zambia dakika ya 87.

Mechi za Kundi A zinakamilika Jumapili usiku Mali wakichuana Zimbabwe nao  Burkinafasso wapimane nguvu na  wenyeji Cameroon .

Mechi hizo zitabaini timu mbili zitakazofuzu kwa robo fainali ya Jumamosi na Jumapili ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *