Tanzania yakanusha madai kwamba hospitali zake zimejaa wagonjwa wa korona

Wizara ya Afya nchini Tanzania imekanusha madai yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba hospitali nchini humo zimejaa wagonjwa wanaougua COVID-19.

Katibu wa kudumu katika wizara hiyo Profesa Mabula Mchembe ameonya umma dhidi ya kusambasa taarifa hizo zinazosababisha hofu miongoni mwa raia.

Profesa Mchembe amesema kuwa amezuru hospitali mbili kuu za Mloganzila na Muhimbili jijini Dar es salaam na ameridhika kwamba sio kila mgonjwa aliyelazwa katika hospitali hizo anaugua ugonjwa wa COVID-19 jinsi inavyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Serikali ya Tanzania imeshutumiwa mara kadhaa kwa kujaribu kuzima habari kuhusiana na ugonjwa wa COVID-19.

Mapema wiki hii, Waziri wa Afya wa nchi hiyo Dorothy Gwajima alitoa taarifa ya kuonya mashirika ya habari dhidi ya kuchapisha habari zisizo rasmi kuhusiana na maambukizi ya virusi hivyo.

Kwenye taarifa hiyo pia, Gwajima alisema taifa hilo halina mipango ya kuagiza chanjo za kigeni za ugonjwa wa COVID-19 na badala yake akawahimiza raia wa nchi hiyo kutumia madawa ya kienyeji kama njia moja ya kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo.

Tanzania ni moja wapo wa mataifa machache duniani ambayo hayachapishi takwimu kuhusu maambukizi ya virusi hivyo.

Mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilihimiza Tanzani kufikiria kuwachanja raia wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *