Tanzania waitemea Djibouti ‘cheche za moto’ CECAFA

Mabingwa watetezi Tanzania wajulikanao kama Ngorongoro Heroes wameanza vyema kutetea kombe la Cecafa baada ya kuwachachafya  Djibouti mabao 6-1 katika mchuano wa ufunguzi wa kundi A uliosakatwa Jumapili alasiri katika uwanja wa Black Rhino Academy Sports Complex.

Wenyeji walijikuta taabani katika kipindi cha kwanza baada ya limbukeni Djibouti kuwafunga bao la dakika ya 14 kupitia  free kick ya  mshambulizi Kassim  na kudumu hadi kipenga cha mapumziko.

Kipindi cha pili Ngorongoro Heroes walirejea kwa vishindo huku Teps  Evans akikomboa bao katika dakika ya 54  naye Abdul Seman akawaweka wenyeji kifua mbele kwa goli la dakika ya 65  akijibu tobwe lililotemwa na kipa wa Djibouti na kurejea kwa bao la tatu kunako dakika ya 72.

Mabao mengine matatu ya Tanzania yalifungwa na Khelfin Salum ,Razack Shekimweli na Abdul aliyefunga penati na kufunga mechi kwa mabao matatu.

Mashindano hayo kuendelea Jumatatu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid  kwa pambano la kundi B Uganda dhidi ya Sudan Kusini saa kumi alasiri ,mechi itakayotanguliwa na ile ya kundi C baina  ya Kenya Rising Stars dhidi ya Ethiopia kuanzia saa saba adhuhuri katika uwanja wa Black Rhino Academy .

Mashindano hayo yanayoshirikisha mataifa 9 yatakamilika Desemba 2 huku timu mbili bora zikifuzu kwa mashindano ya Afcon mwaka ujao nchini Mauritania.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *