Tanasha Donna aandaa tamasha

Mwanamuziki wa Kenya Bi. Tanasha Donna ameandaa tamasha ijumaa tarehe 11 mwezi Disemba mwaka huu wa 2020. Tamasha hilo litaandaliwa katika eneo la Afro sayari jijini Nairobi.

Akitangaza tukio hili kwa mara ya kwanza kupitia Instagram, Tanasha alisema kwamba yeye mwenyewe atakuwa anatumbuiza siku hiyo na atakuwa na mgeni fulani kutoka nje ya nchi ambaye hatamfichua hadi siku hiyo.

Watakaohudhuria tamasha watahitajika kuvalia mavazi ya rangi nyeupe. Kulingana na tangazo la tamasha hilo kwa jina “Tanasha Donna all white party”, kiingilio kwa wageni wa heshima au watu maarufu yaani ‘VIP’ ni shilingi elfu nne na meza ya watu wanne kwa wageni maarufu zaidi yaani ‘VVIP’ itauzwa kwa shilingi elfu ishirini.

Lakini kwenye tangazo la hivi punde zaidi la Tanasha Donna chini ya video aliyochapisha ya meneja wake Jamal Gaddafi, mwanamuziki huyo anasema kuna tiketi za shilingi mia tano na zinaweza pia kununuliwa langoni siku hiyo.

Kulingana na picha za matangazo ya tamasha hilo ambazo Tanasha amechapisha kwenye akaunti yake ya Instagram kuna watu wengi maarufu ambao wamethibitisha kuhudhuria tamasha hilo.

Waliothibitisha kufikia sasa ni kama vile mchekeshaji wa redio Felix Odiwuor au ukipenda ‘Jalang’o’, meneja wa Tanasha Jamal Gaddafi, mwanamitindo na mtangazaji wa Uganda Sheila Gashumba, mwanamuziki wa Kenya Redsan, mwanamuziki Barak Jacuzzi na Karun kati ya wengine wengi.

Waandalizi wanasisitiza kwamba maagizo ya wizara ya afya ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona yatazingatiwa wakati wa tamasha ambapo asiye na barakoa hataruhusiwa kuingia.

Mashabiki wanasubiria sana kuona ikiwa tamasha litatimia na kuwaridhisha baada ya mashabiki kukosa kuridhika na utumbuizaji wa Donna mwezi Februari wakati alikuwa akizindua nyimbo zake kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *