Categories
Kimataifa

Taharuki ya kiusalama yatanda nchini Uganda kabla uchaguzi mkuu Alhamisi

Vikosi vya usalama nchini Uganda vimesema maafisa zaidi wa usalama watapelekwa katika wilaya zote 39 nchini humo ambako kunakisiwa ghasia za uchaguzi zinaweza kuzuka.

Tangazo hilo ni miongoni mwa mikakati ya matayarisho inayowekwa kabla ya uchaguzi mkuu siku ya Alhamisi.

Haya yanajiri huku Tume ya Mawasiliano nchini humo ikiagiza kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano ya mitandao ya kijamii kufungwa.

Miezi miwili ya kampeni imekumbwa na ghasia na kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani na wafuasi wao.

Polisi wanasema malori ya kusafirisha mafuta, magari yanayobeba vilipuzi na malori mengine makubwa hayataruhusiwa katikati ya Mji Mkuu wa nchi hiyo Kampala, siku ya upigaji kura.

Maafisa wa usalama wana wasiwasi kwamba vifaa kama hivyo vinaweza kutumiwa na waandamanaji.

Uegeshaji magari kando ya barabara pia hautaruhusiwa mjini Kampala.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Polisi nchini Uganda, Martin Ochola, alionya kwamba yeyote atakayezua vurugu atajuta.

Maafisa wa serikali wanasema kupelekwa kwa maafisa wa usalama kushika doria kunanuiwa kudumisha amani lakini wahakiki wanaonelea kuwa hilo ni jaribio la kuwahangaisha wapiga kura.

Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kati ya Rais wa sasa Yoweri Museveni na hasimu wake Bobi Wine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *