Categories
Burudani

Wasanii wakesha studioni kuandaa wimbo wa maombolezo

Kufuatia kifo cha Rais wa muungano wa Tanzania jana jioni, wasanii wengi tajika nchini Tanzania waliamua kuingia studioni kuandaa wimbo kwa ajili ya kumlia kiongozi huyo.

Kulingana na picha na video zilizochapishwa na Wasafi Tv wasanii ambao walikuwa studioni kwa pamoja usiku ni kama vile Diamond Platnumz, Khadija Kopa, bintiye Zuchu, Mbosso, Ben Pol, Christina Shusho na wengine wengi.

Marehemu Rais wa Tanzania John Joseph Pombe Magufuli alitambua sana wanamuziki nchini humo kwa kazi yao ambayo wanafanya. Na ndio maana wakati wa kampeni za kutafuta kuchaguliwa tena mwaka jana, alitumia wanamuziki hao kwenye mikutano ya kampeni.

Aliposhinda aliwahusisha pia katika sherehe ya uapisho wake.

Wengi wa wasanii hao pia wamemwomboleza liongozi huyo wa taifa kwa namna ya kipekee kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii. Msanii Harmonize au ukipenda Konde Boy alipachika video inayomwonyesha akiangua kilio kwenye Instagram stories baada ya kupashwa habari kuhusu kifo cha Magufuli.

Harmonize aliwahi kubadilisha wimbo wake ambao alikuwa amefanya na Diamond Platnumz uitwao Kwangwaru na kuuita Magufuli akisifia utendakazi wake.

Sio yeye tu ambaye ana wimbo wa kusifia marehemu Rais, wengi tu walitunga na kuimba nyimbo za aina hiyo akiwemo malkia wa WCB Zuchu.

Categories
Burudani

Baba Levo amshukuru Diamond Platnumz

Mwanamuziki na mtangazaji wa kituo cha redio cha Wasafi Fm nchini Tanzania Revokatus Kipando maarufu Baba Levo anamshukuru mwanamuziki Diamond Platnumz kwa kumsaidia kuendelea umaarufu wake jambo ambalo limemletea mengi mazuri.

Kupitia Instagram mtangazaji huyo aliandika, “KUWA KARIBU NA WEWE IMETOSHA KUNIPA PESA AMABAYO SIKUTEGEMEA KUJA KUISHIKA NA UZEE HUU.. Naomba Niweke wazi Kwa Mashabiki Wangu Kwamba Kabla Ya Mwezi Huu Kuisha Nitakuwa Nimesain Mikataba Na MAKAMPUNI TISA MAKUBWA Yote Yanataka Niwe BALOZI Wao Kwenye Bidhaa Zao Tofauti Tofauti… Niseme Tena ASANTE @diamondplatnumz Asante Sanaaa..”

Diamond alijibu usemi huo wa Baba Levo akimwita “Fundi Majumba” na kisha kuweka ishara ya moto na kilipuzi kuonyesha kwamba amekubali shukrani zake.

Wiki tatu zilizopita msanii huyo alizua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii kwa kusema kwamba yeye angekuwa mwanamke kama Zuchu, angemzalia Diamond watoto watatu.

Usemi huo ulisababisha wengi kumrejelea Baba Levo kama chawa jina ambalo analikubali kwa kuwa mara nyingi huwa yuko karibu sana na Diamond Platnumz ambaye ni mkubwa wake kikazi.

Huwa anazungumzia utajiri wa Diamond Platnumz hadharani huku akisema kwamba anakubali kamzidi kifedha lakini atatumia umaarufu wake ili naye aendelee.

Categories
Burudani

Lava Lava kuzindua nyimbo zake Kesho

Mr. Love Bite mwanamuziki wa Tanzania ambaye anajulikana na wengi kama Lava Lava ametangaza kwamba kesho Ijumaa ataachilia msururu wa nyimbo zake ambazo kwa jumla amezipa jina la “Promise”.

Kazi hiyo ambayo inalenga msimu wa mapenzi kwani nyimbo nyingi ni za mapenzi itazinduliwa kesho tarehe 12 mwezi Februari mwaka 2021 huku siku ya ya wapendanao ikiadhimishwa jumapili tarehe 14.

Lava Lava ambaye jina lake halisi ni Abdul Juma Idd, amepachika picha ya nje ya kazi hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram na kulingana naye, orodha kamili ya nyimbo hizo itatolewa kesho pia.

Lava Lava alijiunga na Wasafi Classic Baby ya Diamond Platnumz mwaka 2015 lakini akatangazwa rasmi mwezi mei mwaka 2017 wakati wa kuzindua kibao chake kwa jina, “Tuachane”.

Alitangulia kuzindua audio ya kibao hicho na siku mbili baadaye akazindua video yake.

Kabla ya kujiunga na WCB, Lava Lava na Mbosso walikuwa marafiki wa karibu lakini baadaye ukaribu huo ukatoweka na ndipo mashabiki wao wakaanza kukisia kwamba wamekosana.

Lakini alipohojiwa mwezi Oktoba mwaka 2020, Mbosso alielezea kwamba wanamuziki wa WCB huwa hawaonekani pamoja mara nyingi kwa sababu kila mmoja hufanya kazi zake binafsi na wanakutana wakati wa kuwasilisha kazi hizo.

Jambo lingine ambalo alifichua ni kwamba wanamuziki wote hupiga kura ili kuchagua kibao ambacho kitazinduliwa mwanzo.

Kulikuwa pia na usemi kwamba Zuchu anapendelewa sana na usimamizi wa WCB kuliko wanamuziki wengine ambao wanasimamiwa na kampuni hiyo.

Categories
Burudani

Zuchu balozi wa utalii Zanzibar!

Zuhura Othman Soud maarufu kama Zuchu anaendelea kupaa katika kazi yake ya uanamuziki ambayo imemletea mengi mazuri. Mwanamuziki huyo wa kundi la WCB ambaye hajamaliza hata mwaka mmoja katika kazi ya muziki sasa ameteuliwa kuwa balozi wa utalii kisiwani Zanzibar nchini Tanzania.

Kisiwa cha Zanzibar kinajisimamia kwa kiwango kidogo na kina serikali yake ambayo inaongozwa na Rais Daktari Hussein Ali Mwinyi na kuna baraza la mawaziri lakini kijumla kisiwa hicho ni himaya ya Tanzania ndiposa serikali ya Tanzania inaitwa “serikali ya muungano”.

Zuchu alichapisha cheti cha uteuzi huo ambacho alipokwezwa na waziri wa utalii kisiwani Zanzibar Bi. Lela Muhamad Mussa. Alitangazwa kwenye kikao na wanahabari cha kuzindua rasmi kampeni ya usafi kwa lengo la kuimarisha utalii kisiwani Zanzibar.

Binti huyo wa mwanamuziki Khadija Kopa ambaye ni mzaliwa wa kisiwahich cha Zanzibar ni mwingi wa furaha kwa kupatiwa kazi hiyo huku akiahidi kwamba atatangaza vivutio vya utalii kisiwani humo ulimwenguni kote.

Kwenye video aliyochapisha, yeye na wengine kama waziri Lela wanaonekana ufuoni ambapo wanadhamiria kuhakikisha usafi wa hali ya juu na kuvutia watalii zaidi.

Kibao cha hivi karibuni kutoka kwa Zuchu kwa jina ‘Sukari’ kimependwa na wengi huku kikipata kutazamwa mara nyingi kwenye mtandao wa You Tube na kusikilizwa na wengi pia kwenye majukwaa ya kuuza muziki mitandaoni.

Categories
Burudani

Kibao cha Harmonize na Anjella kuzinduliwa siku ya wapendanao

Harmonize anayemiliki kampuni ya wanamuziki kwa jina Konde Music aligonga vichwa vya habari mwishi wa mwaka jana baada ya kuomba kufanya kazi na msanii anayeibukia nchini Tanzania kwa jina Anjella.

Anjella anaishi na ulemavu na amekuwa tu akitumbuiza kwa kurudia nyimbo za wasanii wengine wakubwa na hapo ndipo Harmonize alifurahishwa na uwezo wake wa kuimba.

Kinyume na matarajio ya wengi Harmonize msanii mkubwa alimtumia Anjella ujumbe kwenye Instagram akimwomba afanye kazi naye jambo ambalo Anjella hakuamini.

Lakini baadaye wasanii hao wawili walikutana na kuanza kupanga mikakati ya kushirikiana kikazi na kazi hiyo inaonekana kukamilika kulingana na tangazo la Harmonize kwamba kibao chao kitaanguka tarehe 14 mwezi huu wa Februari siku ya wapendanao.

Awali Harmonize alikuwa amepanga kwamba kazi yake na Anjella iwe ya kwanza ya mwaka huu lakini anaonekana kubadili mipango kwani tayari amezindua wimbo mwingine kwa jina “Anajikosha” na amemhusisha Anjella kwenye video.

Wimbo wao unaitwa “All Night” na kwenye tangazo lake, Harmonize anadai kwamba ni wimbo mzuri sana na utamuinua Anjella sana. anamshukuru pia kwa kazi yake na kukubali kufanya kazi naye.

Harmonize amebadilisha muonekano wa Bi. Anjella ambaye awali alikuwa anavaa tu kawaida na hakuwa anatumia vipodozi.

Anjella alivyokuwa akionekana awali na anavyoonekana sasa

Wanaofuatilia muziki nchini Tanzania wanaonelea kwamba hatua ya Harmonize ya kuleta Anjella na kufanya naye kazi ni ya kujaribu kushindana na Diamond Platnumz ambaye alimchukua Zuchu akaanza kufanya naye kazi na sasa Zuchu anafanya vywema.

Awali Harmonize alikuwa chini ya usimamizi wa Diamond kwenye WCB lakini akagura na kuanzisha kampuni yake ya muziki kwa jina “Konde Music”. Kila mara huwa anatoa nyimbo na kusema maneno ambayo wengi huwa wanahisi yanamlenga Diamond ila Diamond hajawahi kujibu.

Wakati mmoja Harmonize alikiri heshima na mapenzi yake kwa Diamond na Diamond hakujibu. Juzi juzi akihojiwa kwenye kituo cha Wasafi Fm, Diamond alisema hakujibu utambuzi wa Harmonize kwani alihisi kwamba yeye sio mkweli na huwa anatumia jina lake kujitafutia umaarufu.

Categories
Burudani

Sukari, Zuchu

Zuchu mwanamuziki anayeangaziwa zaidi katika kampuni ya WCB nchini Tanzania ana kibao kipya kwa jina “Sukari” ambacho alikiachia rasmi kwenye You Tube tarehe 20 mwezi Januari mwaka 2021.

Wimbo huo ulikuwa umesubiriwa kwa hamu na ghamu kutokana na namna alikuwa amefanya matayarisho ya ujio wake kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram.

Alitafuta usaidizi wa watu kadhaa maarufu nchini Tanzania ambao wana umuhimu kwenye jamii kwa jumla ambao walirekodi video fupi kuhusu wasifu wao na mwisho wote wanamalizia kujirejelea kama sukari.

Mamake mzazi ambaye pia ni msanii kwa jina Khadija Omar Kopa ni kati ya waliosaidia kutangaza ujio wa kibao hicho cha Sukari. Kwenye video yake, Khadija anasifia burudani yake ambayo anasema ikosekanapo watu hutaharuki na watu huwa tayari kuigharamia wakati wowote. Onyesho zuri la usaidizi wa mama kwa mwanawe hasa katika kuendeleza talanta.

Mwingine kati ya watu hao mashuhuri ni muigizaji Wema Sepetu ambaye alisema kwamba urembo wake ndio ulimjengea jukwaa analosimamia kwa sasa tangu mwaka 2006 baada ya kushinda shindano la ulimbwende wakati huo na kutawazwa “Miss Tanzania”.

Aligusia pia kipaji chake cha uigizaji ambacho anasema ni cha hali ya juu zaidi na kwamba yeye ni sukari.

Kabla ya kuachilia kibao hicho, Zuchu naye alitoa video akisema kwamba anaamini kila mwanadamu ana umuhimu wake katika jamii. Umuhimu huo ndio anafananisha na ladha ya sukari huku akijirejelea kama sukari ya Zanzibar alikozaliwa.

Zuchu alikwenda kuhojiwa katika kituo cha redio cha Wasafi Fm katika kipindi cha jioni kwa jina Mgahawa ambapo alionyesha waliokuwepo jinsi ya kuuchezea wimbo huo.

Ikumbukwe kwamba alipoingia WCB alimhusisha mkubwa wake Diamond kwenye nyimbo kadhaa ambazo zilisababisha minong’ono kwamba wana uhusiano wa kimapenzi.

Walikuwa wakiandamana kwenye maonyesho kadhaa lakini zamu hii Zuchu alikuwa peke yake alipokwenda kuhojiwa. Alisema Diamond alimpa ahadi ya kumshika mkono alipokuwa akianza lakini pia alimwambia kwamba kuna wakati atamwachilia afanye kazi peke yake.

Kama ilivyo mazoea nchini Tanzania, wengi wamerekodi video wakichezea wimbo huo mpya wa Zuchu kwa jina sukari na amechapisha hizo video kwenye akaunti yake ya Instagram.

Categories
Burudani

Niko sawa! Zuchu awambia mashabiki

Malkia wa kampuni ya wanamuziki nchini Tanzania Wasafi Classic Baby WCB Zuchu amewaarifu mashabiki wake kwamba yuko salama salmini. Hii ni baada ya msanii huyo kuanguka akiendelea kutumbuiza huko Dodoma jana usiku.

Alikuwa kwenye tamasha la Wasafi Media na alianguka alipojaribu kukwea ngazi moja ambayo ilikuwa nguzo ya jukwaa la muda ambalo walikuwa wakitumia.

Hata hivyo aliinuka kwa haraka na kupanda kwenye chuma hizo na kuendelea kucheza huku akishangiliwa na mashabiki.

Lakini wafuasi wake wamekuwa wakimkejeli kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakihofu kuhusu usalama wake baada ya ajali hiyo.

Kwa sababu hiyo, Zuchu akapachika picha kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa amevalia mavazi alokuwa amevaa wakati akitumbuiza na kushikilia bunda la pesa kana kwamba ni rununu na kuandika maneno haya; “Hello Ambulensi, niko salama msijali.”

Mtumiaji mmoja wa Instagram kwa jina ‘Carrymasttory’ aliweka picha ya Zuchu na kuandika, “Nipo hospitali ya mkoa wa Dodoma hapa hadi muda huu hajaletwa akiwa anaumwa hata maumivu tuu, kumbe kamekomaa eeehhh?”

Carrymasttory huwa anachambua watu maarufu nchini Tanzania pamoja na matukio mbali mbali nchini humo.

Zuchu ambaye hajamaliza hata mwaka mmoja katika kundi la WCB amepata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania na kufikia sasa ameteuliwa kuwania na kushinda tuzo kadhaa ndani na nje ya Tanzania.

Categories
Burudani

Octopizzo apendekezwa kuteuliwa kuwania tuzo za Grammy

Octopizzo ambaye ni mwanamuziki wa nchi ya Kenya ana raha baada ya kupiga hatua katika sanaa yake. Hii ni baada ya kupendekezwa kuteuliwa kuwania tuzo za kifahari za nchi ya marekani za Grammy.

Mwanamuziki huyo kwa jina halisi Henry Ohanga sasa yuko kwenye orodha ya wasanii wanaofikiriwa katika kuwania tuzo za Grammy mwaka 2021.

Hii huwa hatua ya kwanza katika tuzo hizo na baada ya hapo washirika katika “Grammy Academy” watapiga kura kuteua wawaniaji wa tuzo kutoka kati ya wengi waliopendekezwa.

Wimbo wake kwa jina “Another Day” unapendekezwa kuwania tuzo la rekodi bora ya mwaka, huku “Kamikaze ukipendekezwa kuwania tuzo la “Best melodic rap” pamoja na huo wa “Another day”.

Wimbo wake ambao amehusisha Sailors kwa jina “Che che” unapendekezwa kuwania tuzo la “Best Rap Performance”.

Octopizzo alitangaza hayo kupitia akaunti yake ya Twitter.

Wasanii wa Afrika Mashariki ambao pia wako kwenye orodha ya wanaofikiriwa kuwania tuzo za Grammy ni wanamuziki wa kampuni ya Wasafi au ukipenda WCB nchini Tanzania, Diamond Platinumz, Zuchu, na Rayvanny.

Nyimbo za Diamond “Jeje” na “Baba Lao” zinapendekezwa kuwania tuzo la Video bora ya mwaka huku albamu ya Rayvanny kwa jina “Flowers” ikipendekezwa kuwania tuzo la Albamu ya muziki wa dunia bora ya mwaka.

Zuchu anapendekezwa kwa kuwania tuzo la mwanamuziki bora mpya.

Alipohojiwa na Grammys Diamond alisema ikiwa atashinda tuzo la Grammy kwanza ataomba na kushukuru Mungu kwa wiki nzima kisha aandae onyesho kubwa bila malipo nchini Tanzania.

Categories
Burudani

Zuchu ateuliwa kuwania tuzo za Burudani Afrika huko Marekani.

Kitinda mimba wa sasa wa WCB yaani Wasafi kampuni ya muziki inayomilikiwa na Diamond Platinumz ameshapata uteuzi wake wa kwanza kuwania tuzo za kimataifa ilhali amejitosa ulingoni mwaka huu tu.

Zuchu kwa jina halisi Zuhura Kopa ameteuliwa kuwania tuzo katika kitengo cha msanii mpya bora yaani ‘Best New Artist’ katika tuzo hizo zinazojulikana kama “African Entertainment Awards USA”.

Anaoshindana nao ni Masauti wa Kenya, Daddy Andre na John Blaq wa Uganda na Olakira wa Nigeria kati ya wengine.

Masauti, msanii wa Kenya

Bosi wake Diamond ameteuliwa katika kitengo cha mtumbuizaji bora na anashindana na Rayvanny na Harmonize wa Tanzania, Yemi Alade, Tiwa Savage, Burna Boy na Wizkid wa Nigeria, Innos B wa Congo, Eddy Kenzo wa Uganda na Jah Prayzah wa Zimbabwe.

Tuzo za “AEAUSA” zilianzishwa mwaka 2015 kwa lengo la kutambua ufanisi wa Afrika katika nyanja mbali mbali hasa burudani, ujasiriamali na uongozi.

Tuzo zaidi ya 30 hutolewa kila mwaka kwa hafla ya siku katika jimbo la New Jersey Marekani. Hafla ya mwaka huu wa 2020 itaandaliwa tarehe 12 mwezi Disemba.

Categories
Burudani

Zuchu afurahia kukutana na babake mzazi

“Mwaka 2020 ndio mwaka naupenda zaidi maishani. Babangu mzazi. Mwenyezi Mungu atuweke karibu leo mpaka milele. Amani ambayo ninahisi hakuna anayeelewa. Sijawahi kujihisi mkamilifu hivi. Yaliyopita yamepita Mungu atingoze kwenye yajayo. Ninafurahia sana.”

Ni tafsiri tu ya maneno aliyoandika Malkia wa lebo wa muziki ya Wasafi nchini Tanzania Zuchu kwenye picha yake na babake mzazi.

Zuchu anafurahia kukutana na babake mzazi kwa jina “Othman Soud” aliyejitokeza maajuzi na kutangaza kwamba yeye ndiye baba mzazi wa Zuchu.

Hata baada ya kujulikanisha hilo, Othman alisema anajizuia kumtafuta bintiye kwani wengi wataona kwamba anataka kushiriki ufanisi ambao Zuchu amepata maishani baada ya kutokuwa naye kwa muda mrefu.

Zuchu kwa jina lingine Zuhura Othman ni mtoto wa muimbaji wa taarab bi Khadija Kopa. Wakati wa mahojiano, Bwana Othman alimsihi Khadija asiwe kikwazo kati yake na binti yake.

Ishara kwamba Khadija amekuwa akizuia uhusiano wa karibu kati ya Zuchu na babake mzazi. Alipohojiwa miezi kadhaa iliyopita, Khadija Kopa alisema kwamba muziki wake unamlipa vizuri kiasi cha kumwezesha kulea watoto wake kuonyesha kwamba alikuwa akiwalea pasi na baba yao.

Mashabiki wa Zuchu wamemsifia kwa hatua yake ya kwenda kukutana na babake mzazi, kumsamehe na kumwonyesha mapenzi kwani siku zote damu ni nzito kuliko maji.

Zuchu ameinula katika ulingo wa muziki nchini Tanzania mwaka huu baada ya kujiunga na kampuni ya muziki ya WCB au ukipenda Wasafi ambayo inamilikiwa na Diamond Platinumz.